Tunaishukuru serikali kwa kuwa na sikio la kusikiliza na kupokea maoni ya wadau hawa, ambayo kwa nyakati tofauti tofauti yamekuwa yakiwasilishwa na taasisi zilizofanya uchambuzi wa sheria hizo na kuonyesha kwa kiasi gani kuna vifungu vinahitaji kurekebishwa ili kuondoa mkwamo kwenye tasnia hiyo muhimu katika jamii.
Baadhi ya vifungu vinavyopigiwa kelele na wadau ni makosa ya kitaalum kuwa makosa ya jinai, mamkala ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), ambaye anaweza kukifungia chombo cha habari kinapodhaniwa au kutuhumiwa kitenda kosa bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria hasa mhimili wa mahakama wenye mamlaka ya kikatiba katika suala la utoaji wa haki.
Pia ni kuwapo kwa vyombo vingi vinavyosimamia taaluma ya habari na wadau wanaona kuna umuhimu wa kuwa na kimoja ambacho kitasimamia ipasavyo.
KIlio cha wanahabari siyo bure, kwa kuwa kuna mahali sheria hizo zinawaumiza hasa kwenye mamlaka ya mkurugenzi na waziri, ambao wakati mwingine huumiza wafanyakazi waliopo kwenye vyombo husika, huku serikali ikikosa mapato ya kodi za mishahara na nyinginezo zitokanazo na biashara husika.
Tunashukuru waziri amesema serikali itashughulikia mapendekezo hayo kwa lengo la kuiwezesha sekta ya habari kuwa rafiki kwa wadau wake, hususan waandishi wa habari.
Kijaji alikaririwa akisema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kwamba sekta ya habari inakuwa rafiki na ni dhamira ya wote kusonga mbele na kufikia malengo ya ufanisi utakaokuwa na faida kwa kila mmoja.
Tangu kupitishwa kwa sheria hizo mwaka 2015 na 2016, wadau hao wamekuwa wakifanya uchambuzi wa sheria hizo na kuwasilisha mapendekezo ya mabadiliko serikalini, na mara kadhaa yamepokelewa, lakini kwa kipindi chote hakukuwa na mabadiliko, hali iliyoendeleza malalamiko ya wadau.
Tunatarajia ushirikishwaji kamilifu kwenye mabadiliko ya sheria hizi, ili kuondoa maumivu ambayo yanakwaza uhuru wa upatikanaji wa taarifa na uhuru wa kujielezwa kwa Watanzania na wanahabari kwa ujumla.
Tunafikiri sasa maoni ya wadau hawa yatasikilizwa na kufanyiwa kazi ili kuona mabadiliko yanatokea kwenye sheria hizo, kwa kuwa lengo ni kuongeza uwajibikaji kwa pande zote na siyo kutaka uwapo wanataaluma ambao hawawajibiki.
Haitarajiwi kuona nyaraka hizo kuhifadhiwa kabatini kama nyingine zilizowahi kupokelewa, na sasa tunatarajia kuona ushiriki wa wadau wote wa habari katika mchakato uliobaki kwa tasnia ina wadau na taasisi nyingi, ambazo zimefanya kazi ya kuhakikisha inaieleza serikali kuhusu nyaraka hizo na umuhimu wa kufanya mabadiliko.
Tunataraji kuona ushirikiano wa dhati kwa serikali na viongozi wake kwa tasnia ya ya habari kupitia vyama vyao pasipo kubakisha wengine nyuma, lengo hili litasaidia kuimarisha ushirikiano kati ya wahusika.
Chombo cha habari kinapofungiwa maumivu siyo kwa wamiliki, bali mnyororo mrefu wa watu ambao wanaishi kwa kipato kinachotengenezwa na chombo husika, kwa kuwa walioajiriwa nao wana wategemezi wao huku wanaofanya biashara na chombo nao wanapata kula yao kwa uwapo wake.
Tunatambua kuwa vyombo hukosea, lakini mchakato wa kuhukumu ufuate taratibu za haki na uwazi, ndiyo maana kilio kikubwa cha wadau kimekuwa kwenye mamlaka makubwa kwa viongozi ambao hufungia vyombo vya habari.
Kama wanahabari tunawajibu wa kuilinda taaluma yetu kwa wivu mkubwa kwa kukemea matendo yoyote ya kuidhalilisha, na kuhakikisha kila mmoja anatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na maadili badala ya kutumia kalamu kuumiza wengine au kuwabeba wengine.
Uandishi wa habari wenye kujali wengine na maslahi mapana ya nchi, ni hatua kubwa kuleta manufaa chanya kwa nchi, kwa kuwa bado jamii ina imani na vyombo vya habari pamoja na matarajio makubwa.