Alisema katika maeneo mengi hivi sasa kumekuwapo matukio ya uchomaji misitu ovyo hali inayotishia uharibifu wa vyanzo vya maji nchini.
Aidha, alitolea mfano kuwa Bwawa la Mindu, mkoani Morogoro, miaka ya nyuma lilitumika kama chanzo cha maji cha uhakika, lakini hivi sasa kutokana na uharibifu wa mazingira pamoja na uchomaji misitu kumekuwapo ukame mkubwa.
Pia, alisema wizara nane zimejipanga kushirikiana kushughulikia kero ya uchaguzi wa mazingira utokanao na kelele za muziki kwenye kumbi za starehe na nyumba za ibada.
Aidha, alikiri kuwa kero ya miaka yote kwa wizara hiyo ni uchafuzi wa mazingira utokanao na makelele katika kumbi za starehe pamoja na nyumba za ibada.
Dunia kwa saa inakabiliwa na uharibifu mkubwa wa mazingira ambao umesababisha mabadiliko ya tabia nchi na sasa majira ya mvua yamebadilika, ongezeko la baridi, joto na ukame wa muda mrefu.
Mathalani, Tanzania inakabiliwa na ongezeko la joto huku mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Ruvuma ikiongoza, huku mvua zikichelewa kunyesha na kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), zinatarajiwa kuanza kunyesha mwanzoni mwa Desemba.
Ni muhimu sasa kutunza misitu kwamba sheria ndogo za kila halmashauri zifanye kazi kuliko kuendelea kuwa nazo lakini utekelezaji haupo, kasi ya ukataji miti kwa ajili ya mkaa na matumizi ya nishati inaongezeka.
Lakini, tunaona ni muhimu wananchi wakawa na nishati mbadala ili waachane na matumizi ya mkaa ambao kwa sasa ni asilimia 80 ya watumiaji, ikiwa hili litafanikiwa basi kasi ya ukataji miti itapungua.
Licha ya kuhamasisha watu kukata miti na kupanda upya ila tujiulize mti unaokatwa sasa ulipandwa miaka mingapi iliyopita na je, inakatwa mingapi kupata mkaa wa kutosha kwa ambaye amejiajiri.
Mathalani, licha ya marufuku ya serikali kukata miti, lakini kwenye barabara zote kuu ikishafika saa 11 jioni ndiyo mkaa unavyotolewa kuuzwa barabarani, na yote hiyo ni miti imeteketea.
Ni muhimu serikali ikafuatilia kwa karibu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha nishati mbadala kama gesi inashuka bei, itawezesha watu wengi kutumia nishati hiyo na kuachana na kuni au mkaa ambayo inateketeza mazingira.
Pia moja ya eneo korofi waziri alilizungumzia ni kelele za nyumba za ibada na sehemu za starehe, hii inaonekana ni fupa gumu lililozishinda mamlaka kwa kuwa sasa tunaona msimamizi naye anageuka kuwa mlalamikaji badala ya kutumia sheria kuchukua hatua.
Nyumba hizi za ibada na sehemu za starehe zipo kwenye maeneo yetu na ujenzi unapoanza unaonekana hata serikali za mitaa wanaona, lakini wakati mwingine nguvu ya fedha hutumika kuhakikisha biashara hiyo inaendelea.
Licha ya kutakiwa kufunga biashara hizo saa sita usiku wapo wanaoendelea, lakini huoni wakichukuliwa hatua kiasi cha wengi kushindwa kulala hasa wanafunzi na wagonjwa.
Miaka ya nyuma baadhi ya watu binafsi na taasisi walijitolea kupanda miti, na kampeni hiyo iliuongezwa na Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Hayati Dk. Reginald Mengi, ambaye alihamasisha wananchi kupanda miti na kutunza mazingiza nchini.
Hamasa hiyo ilisaidia sana kuwa na mwamko kwa watu binafsi, shule za msingi, sekondari na vyuo kupanda miti kwa wingi.
Lakini ni muhimu sheria ya kuzuia shughuli za binadamu umbali wa mita 60 kutoka kwenye chanzo cha maji ikaheshimiwa kwa kuwa ni kawaida shughuli za kilimo kufanyika hadi kwenye kingo za mito na kuharibu mazingira.
Bila kusimamia sheria nchi itaendelea kukabiliwa na ukame ikiwamo upungufu wa maji, na tayari tunaona mgawo wa maji unavyoshika kasi nchini na kwa kuwa umeme wetu ni wa maji basi muda siyo mrefu kiasi cha maji kitapungua kwenye mabwawa.










