Licha ya hali hiyo, watumiaji hao hususan madereva na makondakta wanatakiwa kulipa ushuru wa Sh. 1,000 kwa kila gari linaloingia kushusha na kupandisha abiria na kwa namna eneo lilivyo hakuna hadhi ya kuitwa kituo ambacho serikali inakusanya mapato.
Magari yanayoingia na kutoka kituoni hapo ni yanayofanya safari za Bunju, Posta, Kivukoni, Kariakoo, Morocco, Mawasiliano, Bagamoyo, Mbezi, Madale na Msata. Hali ya geti na barabara ya kuingia kituoni humo ni kero kwa wenye magari, watembea kwa miguu na wenye maduka ya biashara.
Magari yote yanatoka na kuingilia kwenye geti moja, hali inayosababisha msongamano, hakuna taa, uchafu umetapakaa, hakuna maeneo ya abiria kupumzikia na hivyo mvua na jua kuwa vyao. Mbaya zaidi, wakati wa mvua kuna tope jingi na usumbufu mkubwa.
Choo kinachotumiwa ni cha soko na kinamilikiwa na mtu binafsi, jambo ambalo ni usumbufu mkubwa kwa eneo ambalo manispaa inakusanya fedha kila siku, lakini hazirudi kufanya maboresho kwenye chanzo hicho ili kuongeza mapato zaidi.
Watumiaji wa kituo hicho ni mamalishe, wafanyabiashara ndogo, madereva, wasafiri na wanaopokea wasafiri, lakini mazingira magumu yaliyopo humo yanawafanya wengi kutotumia na kuyasubiri magari nje au barabarani.
Manispaa ilipoulizwa na Nipashe, ilisema zabuni ya ujenzi wa kituo hicho na cha Bunju zimeshatangazwa na matangazo yamebandikwa sehemu mbalimbali, ingawa kwa sasa nguvu kubwa imeelekezwa kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Tunaona pamoja na shughuli nyingi za manispaa, lakini lazima vituo vya daladala ambavyo ni chanzo cha mapato vikatazamwa kwa jicho la tofauti ikiwamo kuhakikisha vinakuwa na huduma zote muhimu.
Moja ya vyanzo vya mapato vya serikali za mitaa ni pamoja na vituo vya daladala na mabasi, na haiwezekani iwe ni sehemu ya kukusanya fedha tu bila kurudisha kwa kufanya maboresho muhimu ili kiingize fedha zaidi.
Bado kuna nafasi ya kujenga choo cha kisasa kwa ushirikiano na sekta binafsi, kuliko kusubiri upatikanaji wa fedha ndipo ujenzi uanze, huku watumiaji wakiumia, lakini hakina hadhi ya eneo husika.
Kutokana na miundombinu duni hali ya usafi siyo ya kuridhisha jambo ambalo ni hatari kwa watumiaji wote, na afya zao kuwa hatarini. Ndiyo maana tunaona ni muhimu sana kituo hiki kikaboreshwa kwa kuwekewa miundombinu muhimu ili isiwe ni ng’ombe anayekamuliwa bila malisho licha ya afya yake mbaya.
Kituo hicho ni kimoja kati ya vingi ambavyo manispaa inakusanya fedha, lakini hazirudi kwa ajili ya kukihudumia, lakini bado kuna nafasi ya kuwekeza na fedha ikarudi ikiwa wataweka ofisi na vibanda vya biashara vitakavyowezesha watu kupangisha.
Ni muhimu sana ubunifu wa kuboresha vyanzo vya mapato ukawepo kwa kuwa kukiwa na vituo vizuri kunabadili mwonekano wa eneo husika, kuna kuza maendeleo lakini mapato yatapatikana kwa wingi na rahisi zaidi huku afya za watumiaji zikibaki salama.
Kwa sasa maboresho yamefanyika kwenye baadhi ya masoko lakini kuna maeneo hayajafanyika, kiasi cha miundombinu kuwa mibovu hasa nyakati za mvua na hatarishi kwa afya za watumiaji. Walipa kodi wanataka kuona miundombinu bora kwenye vituo na masoko au sehemu zote za huduma za kijamii, inapokuwa tofauti wanaona kuwa hawakustahili kupata huduma muhimu na itaathiri chanzo cha mapato.