Chanjo ya UVIKO 19 muhimu kwa afya zetu

19Nov 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Chanjo ya UVIKO 19 muhimu kwa afya zetu

TANZANIA imeingia kwenye orodha ya nchi zilizokubali chanjo ya ugonjwa wa corona, na sasa watu wake wanachanja baada ya kuhamasishwa na kuamini kuwa chanjo ni muhimu kwa afya zao.

Hatua ya kuchanja sasa inaonyesha dhahiri kuanza kuondoa dhana potofu iliyokuwapo awali kabla ya uhamasishaji na elimu ya umma, ambayo ilichangiwa na upotoshaji uliokuwa unafanywa na baadhi ya watu.

Kwa sasa viongozi wanaongoza kwa mfano wa kuvaa barakoa kila wanapokuwa kwenye mikusanyiko, na sasa imekuwa siyo jambo la ajabu kwa mtu kuvaa mbele za watu.

Viongozi wameonyesha kwa mfano kwa kuchanja hadharani kiasi cha dozi ya awali kufika nchini ya Jonson and Jonhson kutokana Marekani kumalizika kabla ya Desemba 2, mwaka huu, ambayo ilielezwa ingeharibika. Pia, zimekuja chanjo za aina nyingine mbili za Sinopharm kutoka China, ambazo zinaendelea kusambazwa kwa wananchi wa maeneo mbalimbali nchini.

Tayari wataalamu wa afya wameeleza faida za chanjo kuwa ni kuongeza nguvu ya kinga ya mwili ili kuuwezesha mwili kupambana na maradhi hasa ya UVIKO-19, na siyo kwamba huwezi kupata bali utakuwa katika nafasi ya kupona zaidi kuliko ambaye hajachanja.

Kwa aliyechanja akipelekwa hospitali kwa ajili ya corona ana nafasi kubwa ya kupona au kutozidiwa kwa kuwa askari wa zaidi waliotangulia mwilini wataongeza mashambulizi kwa adui aliyeingia mwili na mwisho kuwa salama.

Yapo maneno mengi kuhusu corona, ambayo siyo kweli kwa kuwa wataalamu wa afya na wanasayansi kwa ujumla wameshathibitisha kuwa chanjo za COVID-19 zilizopitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), hazina madhara kwa binadamu kwa kuwa zimefanyiwa utafiti wa kutosha.

Aidha, maudhi madogo madogo yanaweza kujitokeza baada ya kutumia ambayo huwa ya muda mfupi sana na baadaye yanatoweka, huku wengi wakishauriwa kumweleza mtoa huduma hali ya afya yake kabla ya kupata chanjo.

Kuna umuhimu mkubwa kwa kila kiongozi kuanzia mkuu wa mkoa na wilaya, makatibu tawala wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, makatibu tarafa, katibu kata na watendaji wa vijiji na mitaa kutoa elimu sahihi kwa umma.

Pia, ni wajibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuendeleza jitihada za kutoa elimu kupitia vipeperushi, mabango na ujumbe mbalimbali ambao utawafikia wananchi moja kwa moja na kufanya uamuzi.

Tunaona jitihada za kutumia vyombo vya habar, lakini bado wananchi wanataka kuona viongozi wakiwafuata na hata kuonyesha mfano wa kuchanjwa kwa kuwa wapo ambao hawajachanjwa. Ikiwa tutafanikiwa kuchanja wengi au Watanzania wote, kasi ya maambukizi au kuugua na kuzidiwa itapungua na kuokoa Watanzania wengi zaidi.

Hakuna ubishi kuwa ukichanjwa huwezi kupata UVIKO-19 na ndiyo maana wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari ikiwamo kuvaa barakoa, kuepuka misongamano, kunawa mikono kwa vitakasa mikono au maji na sabuni muda wote. Kila mmoja akiwajibika atahakikisha wa karibu yake naye anapata chanjo na kuondoa dhana potofu dhidi ya chanjo ambayo imekuwapo miongoni mwa watu.

Kwa maisha ya sasa chanjo haiepukiki na tangu watoto hadi utuuzima tumechanjwa chanjo nyingi ambazo hakuna aliyehoji, lakini hii kumekuwa na habari nyingi za kupotosha na huu ndio wakati umuhimu wa kuwapa wananchi taarifa sahihi.

Taarifa sahihi kwa ajili ya wananchi ni muhimu kwa kuwa zitawawezesha kufanya maamuzi, na hizi zinapaswa kutolewa na wataalamu wa afya na kupigiwa chapuo na viongozi mbalimbali ambao wanawafikia wananchi wa ngazi za chini kabisa.

Ikiwa wananchi wote watapata elimu sahihi ya chanjo, tunaamini watafanya uamuzi sahihi ya kuchanja, ili kupunguza madhara ya kuumizwa na UVIKO 19 ikiwa watapata virusi hivyo.

Dunia inateseka kwa sababu ya UVIKO 19 ambao umebadilisha mwenendo wa maisha ya watu, wengi wamefariki na shughuli za kiuchumi kuathirika kwa kiasi kikubwa, na hadi sasa hakuna tiba maalum ya ugonjwa huo bali dawa mchanganyiko hutumika kumsaidia mgonjwa.

Hakuna namna yoyote tunaweza kuepuka chanjo, ni wajibu wetu sasa kukubali au kuchangamkia dozi zilizopo ili kuokoa maisha yetu.