Ligi Kuu Bara irejee na burudani si 'mauzauza'

20Nov 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ligi Kuu Bara irejee na burudani si 'mauzauza'

LIGI Kuu ya NBC Tanzania Bara imerejea tena kuanzia jana kwa timu nne kushuka dimbani kupambana wakati leo Jumamosi mechi nyingine tatu zinatarajiwa kuchezwa kwenye viwanja tofauti hapa nchini.

Mbali na ligi hiyo, pia Ligi Kuu ya PBZ Zanzibar nayo imerejea kuanzia jana na kesho itaendelea kwenye viwanja mbalimbali vya Unguja na Pemba.

Ligi hizo zilisimama kupisha kalenda ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), ambapo mataifa mbalimbali yalikuwa yanapambana kucheza mechi za kusaka tiketi ya kushiriki fainali za mwakani za Kombe la Dunia huko Qatar.

Kwa upande wa Tanzania, Timu ya Taifa maarufu Taifa Stars yenyewe imeshatolewa kwenye kinyang'anyiro hicho baada ya kushindwa kuzichanga vyema karata zake.

Taifa Stars inayonolewa na Kim Poulsen, raia wa Denmark, ilimaliza mechi za hatua ya makundi ikiwa kwenye nafasi tatu ikiwa na pointi nane, nyuma ya vinara Jmahuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), waliofikisha pointi 11, Benin waliokuwa na pointi 10 na Madagascar iliburuza mkia ikiwa na pointi nne.

Mbali na timu za Afrika, pia Ulaya mataifa mbalimbali nao walikuwa kwenye mchakato huo na baadhi ya timu tayari zimeshakata tiketi ya kwenda Qatar huku nyingine sawa na mataifa 10 ya Afrika yakisubiri hatima yao baada ya kucheza michezo ya hatua ya mtoano ambayo itachezwa Machi mwakani.

Hayo yamemalizika, waliofanikiwa wamefanikiwa, na waliokosa tiketi ya kushiriki fainali hizo zinazokuja, bado wana nafasi ya kukaa na kutafakari pale walipokosea ili kuanza kujiimarisha kwa ajili ya mashindano mengine yatakayochezwa 2026.

Tunaamini mbali na Taifa Stars kushindwa kutimiza ndoto zake kama ilivyotarajiwa, lakini kuna baadhi ya mambo ambayo wachezaji, viongozi, wadau na mashabiki wa soka Tanzania wamejifunza kupitia michuano hiyo mikubwa iliyoko mbele yetu.

Nidhamu ambayo ilionekana kwa timu zote zilizokuwa zinashiriki michuano hiyo iwe fundisho kwa wachezaji wa hapa nchini ambao siku moja nao wanatakiwa kupata nafasi ya kupeperusha bendera ya taifa.

Hakuna timu ambayo inaweza kuvuna matokeo chanya kama haikuwa na maandalizi bora au wachezaji wenye viwango vya juu ambao wanaweza kushindana.

Umefika wakati kwa wachezaji wanaoshiriki katika ligi mbalimbali za hapa nchini wakajituma na kucheza kwa bidii ili kuonekana na mawakala wa nje na hatimaye kusajiliwa na timu zinazoshiriki ligi zilizoendelea.

Viwango na ufundi vilivyoonyeshwa na wachezaji wa Afrika wanaocheza kwenye Ligi za Ulaya vimesaidia kwa kiwango kikubwa kuzibeba timu zao, hivyo hilo ni somo kwa nyota wa hapa nchini kuendelea kujituma na kusajiliwa Ulaya na baadaye watakaporejea kuitumikia Stars, wanakuja wakiwa imara na walio tayari kwa mapambano.

Kama ambavyo tumeshuhudia vikao vya maandalizi ya mchezo, namna timu zilivyoingia uwanjani, tunatarajia hayo pia yaonekane kwenye mechi za Ligi Kuu ya NBC Tanzania, Ligi ya Championiship ambazo huzalisha idadi kubwa ya wachezaji wanaoitwa kwenye kikosi cha Stars.

Wachezaji wanatakiwa kuamini soka safi ndiyo huzalisha matokeo chanya na kamwe si kufanya vitendo vya kishirikina kama tutahitaji kufika kule ambapo Waafrika wenzetu kutoka Algeria, Tunisia au Nigeria walipo.

Tutumie kile tulichojifunza katika mechi za kimataifa kuzipa heshima ligi zetu kwa sababu msingi imara wa mchezaji huanzia sasa na si kusubiri ngazi ya juu ambayo ataifikia.