Baada ya kusomwa kwa bajeti hiyo, wabunge watakuwa na nafasi ya kuichambua na kuipitisha tayari kwa kufanyiwa kazi.
Hii itakuwa bajeti ya kwanza tangu Rais John Magufuli, aingie madarakani Novemba 5, mwaka jana.
Itakuwa nafasi kwa wananchi kufahamu dira na mwelekeo wa Serikali ya awamu ya tano ya kuipeleka Tanzania katika maendeleo ya kiuchumi.
Tanzania tangu kupata uhuru wake miaka 54 iliyopita, imekuwa katika vita ya kukabiliana na maadui wakubwa ujinga, maradhi na umaskini.
Mategemeo makubwa ya wananchi na wachambuzi wa masuala ya uchumi ni kuwa bajeti hii itajikita katika utekelezaji wa ahadi za Rais Magufuli na Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Baada ya kuchaguliwa kuingia madarakani, Rais Magufuli na CCM wana deni la kutekeleza ahadi zao.
Na pia bila shaka bajeti hii itakuwa sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa mwaka 2015-2020.
Bajeti inasomwa katika kipindi ambacho taifa linakabiliwa na changamoto ya kupiga hatua kimaendeleo.
Hata hivyo, jambo la kusikitisha ni kuwa Tanzania iko nyuma kimaendeleo licha ya kuwa na rasilimali nyingi kama ardhi yenye rutuba, madini na gesi.
Wananchi walio wengi wanaamini kuwa viongozi na watendaji wa serikali ndio chanzo cha nchi kushindwa kupiga hatua kimaendeleo kutokana na utendaji wa kiwango cha chini.
Rais Magufuli amekuja na mbiu ya `Hapa Kazi tu’ na ameanza kuitekeleza kwa vitendo kama ambavyo imejidhihirisha kwa kuwawajibisha viongozi wazembe na kurudisha nidhamu ya utendaji serikali.
Hata hivyo, bajeti hii ndio itatoa mwongozo wa jinsi serikali ya awamu ya tano itakavyotekeleza majukumu yake ili kuwaletea Watanzania maendeleo.
Tunashauri wabunge waisome na kuichambua bajeti hii kwa ukamilifu ili watoe mawazo yenye tija ya kuisaidia serikali kufanya maboresho.
Hatutegemei mjadala wa bajeti kuongozwa kwa misingi ya vyama bali uzingatie masilahi ya taifa.
Suala la bajeti ni la kitaifa kutokana na ukweli kuwa linagusa maisha kila mwananchi.
Itakuwa jambo la kusikitisha ikiwa mjadala wa bajeti utaegemea zaidi misingi ya siasa za vyama badala ya maslahi ya wananchi.
Ukweli upo kuwa matatizo ya umasikini, maradhi na ujinga yanagusa kila mtanzania na hayatokani na itikadi za vyama.
Mathalani kila mtanzania anayekwenda hospitali hapewi huduma kwa kuzingatia anashabikia chama gani.
Watanzania kwa sasa wanataka kuona taifa lao linasonga mbele kimaendeleo na hasa katika uboreshaji wa huduma muhimu.
Miaka 54, baada ya uhuru, ni aibu kuona bado kuna watoto wanasoma shule bila ya madawati, huduma duni za hospitali na huku watu walio wengi wakipata shida kupata mlo mmoja kwa siku.
Inakumbukwa kuwa wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi kulikuwa na ahadi nyingi za kuifanya nchi yetu kuwa ya neema.
Ahadi hizo zilianzia kwa madiwani, wabunge na hata wagombea wa nafasi ya urais, ambao waliahidi kuibadili nchi kuwa ya neema.
Ndio maana tunaomba katika kipindi hiki cha bajeti, wabunge wawe makini kuhakikisha wanapitisha bajeti itakayoboresha maisha ya wananchi wote.
Kwa kuwa wabunge ni wawakilishi wa wananchi, basi wafahamu wamebeba dhamana kubwa ya kuwaletea Watanzania maendeleo kupitia michango na maoni yao ndani ya Bunge.










