Fedha za bajeti zipelekwe mapema kunakohusika zikafanye kazi

09Jun 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Fedha za bajeti zipelekwe mapema kunakohusika zikafanye kazi

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, jana alisoma bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 bungeni jana, ambayo pamoja na mambo mengine, imejielekeza kuifanya nchi kuongeza uzalishaji wa viwanda ili kuongeza ajira.

Serikali imeandaa bajeti ya Sh. trilioni 29.54 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.

Hii ni bajeti ya kwanza tangu Rais John Magufuli, ashike dhamana ya kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano, Novemba 5, mwaka jana.

Kiasi cha Sh. trilioni 17.72 kimetengwa kwa ajili ya matumizi wakati Sh. trilioni 11.82 kwa maendeleo ikiwa sawa na asilimia 40 ya bajeti. Asilimia 26 tu ya bajeti ya 2015/16 ndio ilitengwa kugharamia maendeleo.

Serikali imetangaza hatua mbalimbali za kuongeza kodi kwa bidhaa mbalimbali na kutangaza kodi mpya ili kuongeza mapato.

Wakati akisoma bajeti hiyo, Dk. Mpango alielezea hatua mikakati ya serikali katika kudhibiti matumizi ili kuliletea taifa maendeleo.

Dk. Mpango alihimiza Watanzania kufanya kazi na kuachana na dhana ya kutegemea misaada kutoka nje.

Watanzania walio wengi kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi kwa mateso makubwa kwa kuaminishwa kuwa nchi kama Tanzania ni masikini na ilipaswa kutegemea misaada ya nchi za nje.

Na hiyo ndiyo ikawa staili ya viongozi wengi kuhalalisha safari za kwenda katika nchi za kigeni ili kusaka misaada `eti’ kwa kuwa nchi yetu ni maskini.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepata mafanikio katika siku za karibuni baada ya serikali kubana watu kulipa kodi kihalali.

Serikali kwa sasa inataka kuona inaongeza nguvu katika ukusanyaji wa kodi ili kupata fedha za kugharamia miradi mikubwa ili kuinua uchumi wa taifa.

Serikali imepanga kubana matumizi na imetoa maelekezo kwa maofisa wa taasisi za umma kutumia fedha na rasilimali za serikali vizuri.

Mambo mengine ambayo serikali imejielekeza ni katika usimamizi na kudhibiti matumizi ya serikali ikiwa ni pamoja na kudhibiti matumizi ya umeme, simu na maji na pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.

Waasisi wa taifa hili Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Karume, ndoto yao kubwa ilikuwa kuifanya nchi yetu kujitegemea.

Ndio maana Mwalimu Nyerere aliweka mkazo katika kilimo na ujenzi wa viwanda kwa kuamini vingechochea maendeleo na kuifanya nchi yetu kutotegemea misaada kutoka nje.

Hayati Karume naye alitumia zao la Karafuu kuiendeleza Zanzibar ndio akaanza mradi wa ujenzi wa nyumba kwa ajili ya watu wake na miundo mbinu.

Bahati mbaya katika miaka ya karibuni viongozi walio wengi waliopewa dhamana ya kuongoza nchi yetu wamejielekeza zaidi katika kujineemesha.

Badala ya kuandaa mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuondokana na aibu ya kuomba omba misaada nchi za nje.

Mathalani serikali ikianza kubana zinazokusanywa na Halmashauri mbalimbali nchini ina maana mapato ya serikali yanaweza kupanda maradufu zaidi.

Bado hapo hatujazungumzia makampuni mbalimbali ya uwekezaji, ambayo yamekuwa yakipewa misamaha ya kodi.
Pia kuna maeneo mengine, ambayo yamekilalamikiwa kama yale ya masuala ya gesi na madini.

Hata hivyo, tunaomba serikali katika mwaka mpya wa fedha ihakikishe kuwa inapeleka fedha za maendeleo mapema katika maeneo husika.

Moja ya udhaifu mkubwa katika utekelezaji wa bajeti imekuwa kucheleweshwa kwa fedha za maendeleo katika wizara na taasisi husika.

Hakuna maajabu yoyote kwa nchi kupiga hatua kimaendeleo kwani vitu vinavyohitajika ni watu kujituma, nidhamu na dhamira thabiti.