Shughuli za kibinadamu kandoni mwa vyanzo vya maji zidhibitiwe

07Jun 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Shughuli za kibinadamu kandoni mwa vyanzo vya maji zidhibitiwe

KUNA taarifa za kustusha kuhusiana na kasi ya uharibifu wa mazingira, hasa katika maeneo yaliyo pembezoni mwa vyanzo vya maji.

Shughuli mbalimbali za kibinadamu zikiwamo za ukatataji holela wa miti kwa ajili ya mbao na pia kilimo na ufugaji usiozingatia utunzaji wa mazingira ni baadhi ya sababu zinazotajwa kuwa chanzo cha kuharibiwa kwa mazingira.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kutokana na uharibifu wa mazingira, kuna uwezekano mkubwa wa kukauka kwa vyanzo mbalimbali vikubwa vya maji nchini ikiwa hatua madhubuti za kukomesha hali hiyo hazitachukuliwa sasa.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu, ndiye aliyetoa tahadhari hiyo kupitia mkutano wake na waandishi wa habari kuhusiana na maadhimisho ya ‘Siku ya Mazingira Duniani’ yanayofanytika Juni 5 ya kila mwaka.

Katika taarifa hiyo, Makamu wa Rais aliwataka Watanzania kushiriki kwa vitendo kampeni za kutunza mazingira, huku akitahadharisha kuwa vyanzo vya mito mikubwa kama Rufiji, Pangani na Ruaha vinaweza kukauka katika kipindi cha miaka 15 ijayo ikiwa uharibifu wa mazingira utaendelea kwa kasi iliyopo sasa.

Miongoni mwa mambo matatu aliyoyaainisha Makamu wa Rais kuwa huchangia uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji ni uchimbaji wa madini usiozingatia taratibu na pia ukataji holela wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni, mkaa na shughuli nyingine za ujenzi.

Aidha, hatua zilizopendekezwa kukabiliana na tatizo hilo ni pamoja na kuundwa kwa kamati za mazingira kuanzia ngazi za vijiji, vitongoji, mitaa, kata na wilaya.

Hizi zinatarajiwa kusimamia vyanzo vya maji, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa mara zote vinabaki kuwa salama.

Nipashe tunaunga mkono jitihada za utunzaji wa mazingira katika maeneo ya vyanzo vya maji.

Tunaamini kwamba zipo sababu zaidi ya dazeni kuhakikisha kuwa kila mmoja anashiriki katika utunzaji wa mazingira, hasa kwenye maeneo ya vyanzo vya maji.

Tunaamini kuwa umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji ungali ukifahamika wazi. Vyanzo vya maji vikiathirika, maisha ya viumbe hai wote huwa shakani. Ni kwa sababu hakuna uhai bila ya kuwapo na maji ya uhakika kukidhi mahitaji ya binadamu, wanyama na mimea.

Kwa mfano, zipo athari za wazi huonekana hata sasa katika maeneo ambayo awali yalikuwa na vyanzo vya kutosha vya maji kabla ya kutoweka kutokana na uharibifu wa kila uchao unaofanywa kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu.

Katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa na mito inayotiririsha maji mwaka mzima, hali sasa imebadilika baada ya maji yake kupatikana kwa msimu na mito mingine hukauka kabisa.

Matokeo yake, wakazi wa maeneo ambayo vyanzo vya maji ni haba, na hasa kina mama, wakilazimika kutumia muda mwingi kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kama kunywa, kupikia na kufulia.

Hali hiyo huchangia kuzorotesha uchumi kwa sababu sehemu muhimu ya nguvu kazi hulazimika kutumia muda mwingi wa siku wakitafuta maji.

Aidha, maji yanapokosekana, uoto wa asili hubadilika na kuwa jangwa, makundi ya wanyama huhama au kupoteza maisha na mwishowe kusitisha shughuli za utalii. Maeneo yenye ukame hukumbwa pia na njaa kali.

Kwa kuzingatio yote hayo, ndipo sisi tunapoona kwamba kuna kila sababu ya kuunga mkono kivitendo rai iliyotolewa na Makamu wa Rais katika kuhifadhi vyanzo vya maji.

Kila mwananchi awe mlinzi madhubuti wa vyanzo vya maji kwa kuhakikisha kuwa maeneo hayo hayaharibiwi na kusababisha jangwa.

Shime, maeneo ya vyanzo vya maji yatunzwe vizuri ili kulihakikishia taifa maji ya uhakika kwa maendeleo ya uahkika pia kiuchumi na kijamii.