...kwenye raundi hii ya kwanza ili kuepuka pilikapilika ngumu za mzunguko wa pili.
Kuongezeka huko kwa ushindani kunaifanya ligi yetu kuendelea kufuatiwa ndani na nje ya nchi hasa kwa mataifa ambayo wachezaji wake wanazichezea klabu hapa nchini.
Hii inaifanya Ligi Kuu Tanzania Bara kuongeza mashabiki wengi kila uchwao jambo ambalo tunaamini muda si mrefu tutaona matunda kwa wadhamini kuongezeka kuanzia kwa klabu shiriki hadi ligi yenyewe.
Hicho ndicho tunachotamani kuona kikitokea kwani kuongezeka kwa wadhamini maana yake ni kwamba maslahi kwa wachezaji yatakua lakini ubora wa soka letu utazidi kuongezeka na kuvutia wachezaji wakubwa zaidi kuja kucheza nchini jambo linaloweza kuifanya kuwa miongoni mwa ligi tano hata tatu bora Afrika.
Hata hivyo, wakati ubora huo ukizidi kuonyeshwa na klabu shiriki, waamuzi sasa wanaonekana kuwa kikwazo kikubwa sana katika nchi hii kwani pamoja na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na klabu, wamekuwa chanzo kikubwa cha kufifisha juhudi hizo jambo linaloweza kuwakatisha tamaa wawekezaji.
Tunasema hayo kutokana na maamuzi mabovu yanayotolewa kinyume cha sheria 17 za soka, hivyo kusababisha baadhi ya timu kupoteza na nyingine kushinda pasipo kustahili, jambo ambalo mwisho wa mchezo kama ukiambiwa kutaja nyota wa mchezo pasipo na shaka utapaswa kutamtaja mwamuzi husika.
Kwa mifano michache tu, mechi kati ya Yanga na Geita Gold FC, Mwamuzi Florentina Zablon na Azam FC dhidi ya Ruvu Shooting iliyochezeshwa na Elly Sasii, tumeshuhudia zikitolewa penalti zisizostahili na kupatikana mabao ya kuamua mechi kwa Yanga na Azam kushinda 1-0, hizo zikiwa ni baadhi tu.
Ikumbukwe alama hizo tatu, mwisho wa msimu zinaweza kuamua bingwa ama timu za kushuka daraja, hivyo Shirikisho la Soka nchini (TFF), Bodi ya Ligi (TPLB) na Chama cha Waamuzi nchini (FRAT), wanapaswa kuchukua hatua kali zaidi kwa waamuzi wote wanaofinyanga sheria za soka ili kulinda juhudi kubwa zinazofanywa na baadhi ya wawekezaji na kuvutia wengine zaidi.
Lakini pia waamuzi nao wanapaswa kutambua, ubovu wanaonyesha katika maamuzi yao kunazidi kuwashusha na kupoteza sifa ya kupangwa kuchezesha mechi kubwa za kimataifa zinazosimamiwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) na lile la kimataifa, Fifa.
Katika hili Nipashe tumekuwa tukikemea mara kadhaa na kuitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini(TAKUKURU), kumulika suala hili kwa makini kwani imekuwa vigumu kwa mashabiki na wadau wa soka nchini kuamini kinachofanywa na waamuzi hawa ni bahati mbaya ama makosa ya kibinadamu.
Kwa haya yanayotendeka katika soka letu, yanatushawishi na sisi kuamini asilimia 75 ya kufinyangwa huku kwa sheria 17 za soka kunafanywa kwa makusudi maalum, mapenzi ama maslahi yao binafsi na si suala la kutokujua sheria jambo ambalo TAKUKURU ikiingia kwa miguu miwili hakika ukweli utajulikana.
Tunaamini kama TAKUKURU italivalia njuga ni wazi hali hii itapungua kama si kumalizika kabisa, lakini kuendelea kulifumbia macho soka letu litazidi kudidimia na juhudi kubwa zinazofanywa na TFF chini ya Rais Wallace Karia, kuonekana ni kazi bure, hatutaki kutumbukia kama ilivyoikumba Ligi Kuu Italia mwaka 2006 kwa vigogo vya soka, Juventus kushushwa daraja kutokana na kashifa ya upangaji matokeo.
Hivyo, ni wakati wa kuchukua tahadhari mapema kwa hatua kali kuchukuliwa kwa wote wanaofinyanga sheria za soka kwani likiendelea kufumbiwa macho siku likilipuka litasomba wengi na kuchafua taswira nzima ya soka letu, lakini tunawaonya kama wapo wanaofanya uchafu huo kuacha mara moja.









