Hatua hii ya TRA ni ya kupongezwa

18Nov 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hatua hii ya TRA ni ya kupongezwa

HIVI karibuni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ilitangaza kuachana na tabia ya ukusanyaji wa mapato kwa njia ya mabavu na kuahidi utaratibu wa sasa kodi itakusanywa kwa mazungumzo na walipa kodi.

TRA kupitia Mwenyekiti wake wa bodi, Mussa Uledi ilisema imeona tabia ya kukusanya kodi kwa kutumia mabavu na vikosi kazi imepitwa na wakati na haina tija kwa wakati huu.

Uledi alisema kwa sasa wafanyabiashara wenye madeni ya kodi wamekuwa wakifanya mazungumzo na mamlaka na kutatua changamoto baina ya pande hizo mbili kwa amani.

Uledi alisema pamoja na kuacha kutumia mabavu kukusanya kodi bado mapato ya mamlaka hiyo yamekuwa yakiongezeka mwezi hadi mwezi hali inayothibitisha utaratibu wa zamani wa kutumia nguvu haukuwa na maana.

Sisi tunaona hiyo ni hatua kubwa na ya kupongezwa kwani utaratibu mpya wa mazungumzo ni wa kujenga zaidi kuliko kubomoa kwasababu utasaidia Watanzania wengi kupata mwamko wa kulipa kodi kwa hiari yao.

Katika awamu ya tano tulishuhudia maduka mengi ya wafanyabiashara yakifungwa na mamlaka hiyo kwa madai kuwa wamiliki hawajalipa kodi hali ambayo ilisababisha wafanyabiashara kuiona TRA kama polisi.

Kikosi kazi kilichokuwa kikitumika kukusanya kodi kwa mabavu kilisababisha kwa kiasi fulani wafanyabiashara kuichukia Mamlaka na kushusha ari ya ulipaji wa kodi kwa hiari hivyo kuondoa vikosi kazi ni hatua nzuri.

Tunawapongeza TRA kwa uamuzi huo kwani kufunga maduka ya walipa kodi kwa madai hawajalipa ni utaratibu usio na tija kwa nchi, iwapo mfanyabiashara huyo ataachwa afanye biashara yake anaweza kulipa deni taratibu na hatimaye kulimaliza.

Hatua ya kumfungia duka au ofisi mfanyabiashara ambaye anadaiwa kushindwa kulipa kodi sio mwafaka kwa kuwa jambo hilo linaweza kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo huku biashara zikiendelea.

Sisi tunaona ili kujenga misingi imara ya watu kulipa kodi kwa hiari, TRA inapaswa kuwa rafiki wa wafanyabiashara kuwa nao karibu, kujua maendeleo ya biashara zao badala ya kufanyakazi kama polisi hali inayosababisha uadui baina ya pande hizo mbili.

Wako wafanyabiashara wanaoshindwa kulipa kodi kutokana na kuanguka kwa biashara walizokuwa wakizifanya kutokana na baadhi ya biashara hizo kuwa za msimu.

Ni kweli wako wafanyabiashara wanaoweza kutumia mwanya huo kutaka kukwepa kodi hivyo mamlaka wafanye uchunguzi kubaini ukweli wa madai ya mfanyabiashara huyo kuhusu kushuka kwa mapato yake.

Hali hiyo itadumisha uhusiano mwema baina ya wafanyabiashara na mamlaka hiyo na kuongeza hamasa ya wananchi kulipa kodi kwa hiari.

TRA inawajibu wa kuwaelimisha watumishi wake kufanyakazi kwa diplomasia zaidi kwa kusikiliza shida za wafanyabiashara na kuzitatua au kuzifikisha kwa wakubwa zao zile walizoshindwa kuzitatua badala ya kuwanyanyasa wafanyabiashara.

Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa akiwahimiza TRA kukusanya kodi bila kuwafungia biashara wafanyabiashara wanaodaiwa wala kuwanyanyasa.

TRA wanapaswa kutembea kwenye maagizo ya Rais kwa kuhakikisha inawaongoza wafanyakazi wake nchi nzima kufanya kazi kwa weledi na kujenga urafiki na wafanyabiashara badala ya kujenga mazingira ya uadui.