Ukiwa unasafiri kwa njia ya barabara unaweza kushuhudia jinsi baadhi ya maeneo yalivyoathirika kwa kukosa mvua baada ya mazao kukauka na wanyama kuhangaika kutafuta malisho na maji ya kunywa.
Hii inatokana na uharibifu mkubwa wa mazingira wa kukata miti ambayo inasaidia kuleta mvua.
Miti inakatwa kwa wingi kwasababu ya biashara ya mkaa na imeshamiri kwa kiasi kikubwa kutokana na malori na pikipiki zilizosheheni magunia hayo yanavyotoka msituni kuyabeba.
Katika kudhibiti hali hiyo, serikali imechukua juhudi mbalimbali kwa kufanya kampeni ya kupanda miti ili kuweza kurudisha uoto wa asili na kuhifadhi mazingira.
Kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022–2032) kwa lengo la kutoa mwongozo wa hatua za kuchukua ili kutatua changamoto za mazingira nchini kwa kuzingatia upekee wa changamoto katika sehemu husika na hatua mahsusi zinazopaswa kuchukuliwa.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis, wakati wa mjadala ulioandaliwa na Benki ya Dunia kuhusu jitihada za Tanzania katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni sehemu ya mijadala katika Mkutano wa 27 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea Sharm El-Sheikh, Misri, anaeleza mpango kambambe huo unaonesha changamoto za mazingira zinazoikabili Tanzania ikiwa ni pamoja na uharibifu wa ardhi; uharibifu wa vyanzo vya maji; athari za mabadiliko ya tabianchi; uchafuzi wa mazingira; ukataji ovyo wa miti na uharibifu wa misitu; upotevu wa makazi ya wanyamapori na bioanuai.
“Uharibifu wa mfumo-ikolojia ya pwani na baharini; uharibifu wa ardhi oevu; usimamizi hafifu wa taka; kuenea kwa viumbe vamizi; na changamoto za mazingira katika miji zimeainishwa katika mpango huo,” alisisitiza Naibu Waziri Khamis.
Mpango huo kabambe unatoa hatua za kimkakati na mahsusi kwa kuzingatia jiografia na mifumo ikolojia ya maeneo husika. Hatua hizo zinazingatia utofauti wa mtawanyiko wa changamoto za mazingira na hatua muafaka zinazopaswa kuchukuliwa na kutoa mwongozo kuhusu usimamizi wa mazingira.
Kupitia ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Uendelezaji Mitaji (LoCAL), serikali imeanza kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika halmashauri tatu za Kondoa, Chamwino na Mpwapwa pamoja na kujenga uwezo wa kitaasisi wa kuhuisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
Wito unatolewa kwa jamii kuhakikisha zinaendelea kutunza na kuhifadhi mazingira kwa kuwa Mabadiliko ya Tabianchi ni halisi na kusisitiza utekelezaji wa sera na mikakati kwa pamoja kwa kesho iliyo bora kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Serikali inaishukuru Benki ya Dunia (WB) kwa kuunga mkono jitihada zake katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.
Itakumbukwa Mpango Kabambe wa Hifadhi ya Mazingira ulizinduliwa Juni 5, 2022 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango.









