Hatua hiyo inatokana na wanaume hao kutokutoa taarifa, hivyo kuamua kukaa nayo moyoni na matokeo yake, matukio ya uhalifu yakiwamo mauaji ya wenzi kuongezeka siku hadi siku. Kutokana na kukithiri kwa hilo, serikali imeweka mfumo saidizi ngazi zote zikiwamo madawati ya jinsia, ili wanaume wawe huru kujitokeza badala ya kuendelea kufanya matukio makubwa ndani ya jamii.
Waziri alibainisha kuwa wanaume wengi hawapendi kutoa taarifa wanapofanyiwa ukatili wanaishia kuvumilia na kwamba wapo wanaotendewa ukatili mkubwa lakini wanaamua kunyamaza. Sambamba na kutoa taarifa, aliwashauri wanaume kutengeneza mitandao yao ili wawe na sauti moja kama wanawake wanavyofanya na sauti zao zinakuwa kubwa.
Dk. Gwajima alisema kuna chama cha kutetea haki za wanaume dhidi ya matendo wanayofanyiwa na wenzi wao lakini hakitumiki ipasavyo kutokana na waanzilishi kupigwa vita na wenzao.
Hata hivyo, baadhi ya wanaume wamejitokeza hadharani na kueleza madhila wanayokutana nayo na kuomba jamii iwasaidie huku wengine wakiishia kuvumilia na wengine kulipiza kwa kufanya matukio ya hatari ambayo yamegharimu maisha ya wake zao.
Kwa sasa matukio ya mauaji ya wapenzi au wanandoa yameongezeka ikiwa ni wastani wa tukio moja hadi mawili kila siku na mengi ni mwanaume kaamua kumuua, kumjeruhi mwenza huku sababu kubwa ikielezwa ni wivu wakimapenzi.
Wakati wanaume wakiwa hivyo, wanawake wamekuwa wepesi kusema na wengine kukimbilia vyombo vya sheria ili kupata haki zao. Hulka ya wanaume kujifanya watu wa kumeza (kunyamaza) na kuvumilia, huku wakiogopa kudharauliwa wakiripoti matukio hayo, ndiyo imezidisha kasi ya mauaji katika jamii.
Wengine huhofia kuonekana wamezidiwa nguvu na wake zao au wametawaliwa kwa kiasi ambacho hawawezi kuamua maisha yao ya kila siku, hivyo kukumbana na kebehi kuwa huenda hawana uwezo wa kipato.
Hakuna ubishi kwamba tangu enzi na enzi mwanamume amejengwa kwamba anapaswa kuwa jasiri, lakini kuendelea kuendekeza kasumba hiyo, ndivyo ambavyo matukio ya ukatili yameendelea kutamalaki katika jamii. Kwa wanaume walioshindwa kuvumilia, wamezikimbia familia hatua ambayo pia imesababisha mateso kwa watoto kwa kulelewa na mzazi mmoja au kujiingiza katika makundi ya uovu.
Pamoja na hayo, kutokana na mabadiliko ya kimfumo duniani, jamii inapaswa kubadilika na kupendana na kwa kufanya hivyo, kutakuwa na amani huku wanawake na wanaume wakiishi kwa amani.
Hata hivyo, kama alivyosema Waziri, wakati umefika sasa kwa wanaume kupaza sauti zao juu ya mambo wanayofanyiwa na wake zao hasa ukatili kwa kupigwa na hata kupata ulemavu wa kudumu. Kwa kufanya hivyo, watapunguza ukatili unaoendelea katika jamii pamoja na matatizo ya kiafya kama vile msongo wa mawazo.