Enyi ndugu TANESCO,

25Nov 2022
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Enyi ndugu TANESCO,
  • utaratibu huu wa kutoa taarifa za umeme uwe endelevu

HADI sasa nchi nzima tuko kwenye mgawo wa umeme. Hilo tena siyo suala lenye jibu la kubahatisha, kwani uhalisia na wenye nyumba wenyewe wameweka mambo hadharani kwamba mgawo huo upo.

 

Na tukirudisha mkanda nyuma zaidi, jambo hilo si geni hata kidogo kwenye jamii yetu inakuwapo, na kisha inatoweka na ndiyo mazingira yaliyotawala miaka nenda rudi tangu zama hizo naachana na umri wa udogo, kisha naingia ujana fulani, hadi tarehe hizi ambazo mabinti zetu wanatuwahisha ng'ambo ya pili tunakuwa mababu tutake tusitake, msamiati wa mgawo wa umeme upo pale pale, ambao nikiutafakari naufananisha na ugonjwa wa malaria, kuusambaratisha ni mtihani kweli kweli, unakuja na kuondoka ndani ya familia, kuanzia kule nilikozaliwa mpaka kikosi kipya ninachokiunda mwenyewe.

Nakumbuka wastani wa miongo miwili na ushehe iliyopita, tukatangaziwa kwamba 'mgao wa umeme sasa baibai, kuonana tena majaliwa.' Lakini, ikasonga idadi fulani ya miaka tukaona majaliwa hayo ya kuonana yamerudi tena, mheshimiwa mgao wa umeme kafika.

Hapo ndipo inatuondolea uaminifu katika kile kipengele cha 'kuonana tena ni majaliwa.'

Kikubwa wenyewe tulichokijengea kisaikolojia, tunapitia likizo fulani, kisha tunarudiana na mpambano wa 'no umeme.'

Naam! Juzi tena, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), baada ya minong'ono kutawala kila kona na kila mtu akinena lake 'kwanini' na 'vipi' za kumwaga, wakaona isiwe tabu, sisi ndiyo tunawajibika na shirika hili ni la umma, kwa maana hiyo mali yao tutake tusitake ni lazima tukawaeleze nini kinachoendelea kwenye taasisi yao wananchi ambao pia wanatumia huduma hiyo.

Ukaitishwa mkutano wa waandishi wa habari, mafundi wa kuchakata hizo taarifa wakaufikishe umma nini kinaendelea kutokana na upungufu huo wa umeme.

Jibu Kuu, likaangukia mlemle walikonena wenzao wasambaza maji walipokabiliana na shinikizo kama hilo la watoa umeme, mtuhumiwa mkuu yule yule ukame na ukosefu wa mvua.

Ni ufafanuzi uliozama zaidi ukiainisha bwana ukame na ubovu wa mitambo kwa kiasi fulani, wamesababisha kutoweka kwa megawati zaidi ya 400 za umeme, kilio kikiangukia kila sekta, kuanzia wazalishaji viwandani na wenzangu na mimi na huduma mbalimbali.

Hakuna namna ya kuendelea kushikana mashati, kwani mtuhumiwa ameshapatikana, ila cha kuongeza hapo tabia ya uungwana ulioonyeshwa na wazalishaji umeme hao kuwafahamisha wamiliki ambao ni umma nini kinaendelea na mzizi mkuu wa shida ni nini.

Kutoa taarifa ni jambo muhimu linalosambaratisha kelele za umma, minong'ono isiyofaa ikiwamo kwenye mitandao ya kijamii na kushikana uchawi.

Hata kama baadhi ya watu watakuwa wanalalamika kutokana na machungu ya umeme, lakini kitendo cha TANESCO kuwatangazia wananchi siku fulani kutakuwa na mgawo sehemu fulani, hii angalau inawafanya watafute kitu kibadala.

Mfano mdogo, mtu yupo Mikocheni anajua Mbagala kuna mgao, basi kama kuna mechi hata ya Kombe la Dunia atatazama mechi hadi inaisha ndipo atarejea, ambapo kama isingekuwa hivyo amerudi tu kuwahi mechi na kukutana na giza, akaanza kulaumu kwa nini asingekaa huko huko hadi mechi iishe.

Kutoa taarifa mbali na kujiandaa inasaidia hata kisaikolojia tu ile kufahamu leo kuwakuwa na mgao. Ni kama vile mtu kakukanyaga halafu anakwambia 'pole', ni kama maumivu yake hayaumi kwa sababu za kisaikolojia tu, tofauti na yule ambaye anakukanyaga halafu anaanza kukulaumu kuwa 'huoni?' au 'kapande taxi' kama unataka starehe.

Kama hili la kutoa taarifa ya mgao wa umeme nawapa heko, waendelee hivyo hivyo, na ni jambo la kupongezwa. Lakini angalizo ni kwamba yale yote ambayo yamewabainisha kuwa ni mapungufu yanayosababisha umeme ambayo yapo kwenye uwezo wa kibinadamu wayafanyie kazi mara moja ili mgao umalizike.

 

 

 

 

 

Top of Form

Bottom of Form

Top of Form

Bottom of Form