Ngumi ni moja ya michezo ambayo imewahi kuitangaza vyema Tanzania, kuliletea taifa sifa na heshima kwa nyakati tofauti.
Mabondia wa Tanzania walifanya vizuri katika mapambano ya kimataifa wakiwa hapa nyumbani au kwenye ardhi ya ugenini, lakini waliibuka mashujaa kwa kushinda mikanda ambayo walikuwa wakiiwania kwenye mashindano husika.
Miaka ya nyuma Tanzania ilishuhudia mabondia wake kama Rashid Matumla 'Snake Boy' akishinda mikanda mbalimbali ya kimataifa na katika siku za hivi karibuni, Hassan Mwakinyo, naye alianza kuipeperusha vyema bendera ya taifa (kabla ya sintofahamu iliyojitokeza hivi karibuni huko alipokuwa Uingereza) na kuanza kuwavutia mapromota kuandaa mapambano.
Mbali na kuwavutia waandaaji hao, lakini pia imeonekana kama sehemu ya kuhamasisha mabondia chipukizi kuupenda mchezo huo, na kurejesha nguvu katika kujiandaa kwa ajili ya kupambana kuanzia ngazi ya riadha na baadaye kuhamia kwenye ngumi za kulipwa.
Baada ya kuona na kubaini mchezo huo ulipoteza umaarufu wake, mapromota kutoka sehemu mbalimbali wameamua kuwekeza ili kuufanya urejee kwenye kasi na nafasi iliyowahi kuushika lakini ikiwapa mabondia heshima pamoja na taifa lao pendwa.
Hakuna ubishi mapambano hayo mbali na kutoa burudani kwa wananchi, lakini pia huwasaidia kiuchumi mabondia na wote wanaoshiriki kwa namna moja au nyingine kwenye uandaaji, kwa maana halisi husaidia kutengeneza ajira kwa kada mbalimbali.
Inafahamika lengo kuu la kuandaa mapambano hayo ni kuwatangaza wachezaji hao, kuwapa mazoezi sahihi kuelekea mashindano ya kimataifa yaliyoko mbele yao lakini kuwaongezea kipato kupitia ada wanazolipwa kwa makubaliano rasmi kabla ya kupanda ulingoni, lakini katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia baadhi ya mabondia wakipanda ulingoni mara kwa mara.
Ili kuulinda mchezo husika, ni vyema wasimamizi wa mchezo huo wakahakikisha kanuni, sheria na taratibu hazikiukwi na kwa kufanya hivyo, itawasaidia mabondia kulinda vipaji pamoja na afya zao, badala ya kuweka mbele maslahi ya leo.
Endapo wasimamizi watakaa kimya na kuruhusu mabondia au bondia kuonekana anavunja sheria kwa sababu ya 'njaa' yake binafsi au kwa ushawiki wa promota, jambo hilo lisiachwe liendelea kutoka kwa afya ya maendeleo ya mchezo huo wa ngumi.
Kwa sasa kuna mabondia ambao wameshakuwa maarufu na hawako tayari kuona wanapanda ulingoni mara kwa mara kwa sababu wanafuata kanuni, lakini wapo mabondia chipukizi ambao hawana umaarufu, nao pia wanatakiwa kulindwa kwa kutopata vibali vya kupanda ulingoni nje ya muda sahihi unaotakiwa kutoka pambano moja hadi pambano linalofuata.
Haitakuwa busara pia kuacha kuwapongeza wadhamini na mapromota ambao wanajitokeza kuandaa mapambano mbalimbali kwa sababu wamesaidia kuongeza hamasa katika mchezo huo ambao miaka mitano iliyopita ulionekana kufifia hapa nchini.
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imekuwa ikisisitiza kila idara kutimiza majukumu yake ipasavyo, hivyo kuheshimu taratibu ni moja ya mwongozo ambao serikali kupitia wizara hiyo imesema kwa ajili ya kuhitaji kupata matokeo chanya kwa wanamichezo wake katika kila mashindano watakayoshiriki.
Tunaamini kila mtu atakapofanya majukumu yake kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu, basi malengo yaliyodhamiriwa ya kuuendeleza mchezo wa ngumi yatafikiwa na hatimaye kupata vipaji vipya vitakavyoiletea nchi medali mbalimbali na si kupigana kwa lengo la kunufaisha mapromota au kumaliza tatizo la leo la bondia husika.









