Matukio ya ukatili ni pamoja na vipigo, udhalilishaji na ushambuliaji wa aina yoyote kwa jinsia zote hasa watoto.
Mara nyingi matukio ya watoto kutotendewa haki yamekuwa yakiripotiwa katika vyombo mbalimbali vya habari na vitendo vingine husababisha watu kuamua kujitoa uhai ili kuepukana na mateso wanayoyapitia.
Mijadala inaendelea sehemu mbalimbali kuona namna ya kukomesha vitendo hivyo kwa ushirikiano badala ya kuiachia taasisi moja kupambana navyo.
Ukatili unatokea nyumbani, kazini na maeneo mengine ambayo watu hukutana kufanya shughuli ziwe za kibiashara na nyingine za kujipatia kipato.
Matukio hayo yanaweza kuwa ya udhalilishaji kwa upande wa ajira. Kwa mfano mtu anapotafuta ajira akaambiwa lazima atoe kitu fulani ndipo aipate. Udhalilishaji huo ni sehemu ya ukatili ambao humfanya mhusika kukosa amani na haki yake ya kuwa huru anapokuwa sehemu yake ya kazi.
Unyanyasaji majumbani pia ni ukatili na hutokea kwa watoto, wanaume na wanawake, lakini wengine huogopa kujitokeza kulalamika kwa hofu ya kuchekwa.
Wanasaikolojia wanazungumza kila siku kuwa mtu anapopatwa tatizo linalomsumbua iwe kiakili, kimwili ni vyema akajitokeza na kulisema kuliko kubaki nalo moyoni likiendelea kumuumiza.
Katika siku za hivi karibuni matukio mengi ya watu kujitoa uhai yanasababishwa na wengi wao kushindwa kuliongelea hadharani na kuamua kuchukua hatua za kujiondoa uhai.
Juzi katika mjadala uliokutanisha wanaume katika jukwaa moja mtandaoni, walikuwa wakijadili jinsi wanaume wengi wanavyonyanyasika kwenye nyumba zao kwa sababu ya kutokuwa na uwezo kiuchumi matokeo yanayosababisha hata watoto kumdharau na kwa kuwa mama ndiye anayeendesha familia hiyo, watoto humpa heshima yeye.
Hayo ni baadhi ya matukio yanayoendelea kwenye baadhi ya familia na wengine hudiriki hata kupigwa na wake zao kwa kuwa tu hana uwezo kiuchumi.
Ukatili mwingine hutokea kwa wasaidizi wa ndani ambao huachiwa jukumu kubwa la kuangalia watoto wakati wazazi wanapokwenda kazini.
Wasaidizi hao huwa wa kwanza kuamka na wa mwisho kulala na wengine hawapati chakula kizuri kwa kupewa makombo yaliyoachwa uwe mlo wake.
Wengine huambulia vipigo visivyokwisha kwa sababu tu amekuja pale kufanyakazi na kuonekana ana shida ambayo haiwezi kumuondoa na kulazimika kuvumilia.
Katika siku hizo 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, mambo yote haya hujadiliwa na jamii inatakiwa kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa inapogundua kuwa nyumba fulani kuna tukio ambalo linakwenda kinyume na haki ya binadamu.
Kwa kufanya hivyo, watu wanaonyanyasa au kutowatendea sawa binadamu wenzao watakaogopa na kuacha kufanya vitendo hivyo.
Kila mtu awe mlinzi wa mwenzake ili inapotokea unyanyasaji wa aina yoyote, aweze kuripotiwa na kukomesha unyanyasaji wa aina yoyote ile.
Kila mwaka siku hizi 16 huadhimishwa, lakini kuna baadhi ya watu wanaonekana hawajapata elimu ya kutosha. Hivyo siku hizo ziwe msaada mkubwa wa kuelimisha jamii kuepuka vitendo hivyo.