Waamuzi Bara wameshindikana, wachezaji sasa chukueni hatua

09Jan 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waamuzi Bara wameshindikana, wachezaji sasa chukueni hatua

WAAMUZI ni sehemu muhimu kwenye mchezo hasa kutokana na kusimamia sheria 17 za mpira wa miguu ambao unafuatiliwa na watu wengi zaidi duniani, hivyo ipo wazi kuwa Ligi Kuu Tanzania Bara imekuwa kwenye ushindani mkubwa na kila siku hatua moja inapigwa kuyafuata matarajio.

Hata hivyo, kuna baadhi ya mechi ambazo haki imetoweka kutokana na waamuzi kushindwa kusimamia vema sheria hizo kwa usawa. Makosa yapo kwa wachezaji na waamuzi lakini isiwe kwa kurudia mara kwa mara hasa kwa wakati huu ambao timu ikikosa pointi hata moja inaachwa kabisa kwenye mbio za ubingwa, kumaliza nafasi za juu na kuepuka kushuka daraja.

Katika hili, kwa kuwa mara nyingi jicho la watazamaji ama mashabiki huwaangukia zaidi waamuzi, sisi tunaona ni wakati sasa kwa wachezaji wenyewe kwa wenyewe kuona umuhimu wa kulindana afya zao ili kila mmoja aweze kufikia matarajio yake na ya timu kwa ujumla.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba kwenye mechi ambazo zimepita kuna rafu mbaya ambazo zimewasababishia baadhi ya wachezaji kukaa chumba cha majeruhi wakiuguza majeraha yao kutokana na tu maamuzi mabovu ya waamuzi kwa kushindwa kuchuakua hatua mapema uwanjani.

Matokeo yake, Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), inakuwa ikiishia kupelekana kwenye kamati ya maamuzi na matokeo yake baadhi kufungiwa, wakati huo kuna klabu ambazo tayari zimeshaathirika kwa kupoteza alama ama wachezaji wake kuwa majeruhi.

Pamoja na adhabu hizo, bado makosa yanayofanywa na waamuzi ni yale yale kila uchao, hivyo umefika wakati sasa wa kuwataka wachezaji kutafakari kwa kina zaidi kabla ya kucheza rafu zakuumizana zisizo na maana uwanjani.

Hilo litawafanya wazidi kupata kile kilicho bora na kwa namna soka linavyozidi kukua umakini wao utawapa thamani na kuwa bora kwenye kazi yao, na kuepusha kelele kwa waamuzi ambao wamekuwa wakisemwa kila uchao.

Kila kitu kinawezekana ni suala la muda na kila mmoja kuchukua hatua kwa kujiuliza kwanza kama rafu anayomchezea mwanzeke angefanyiwa yeye ingekuwa sawa?

Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba tunatamani kuona mpira ukichezwa na 'ball' ikitembea na si kushuhudia viatu na rafu mbaya zisizo na afya kwa wachezaji uwanjani.

Tunatambua mambo mengi uwanjani hufanyika kwa kasi zaidi jambo ambalo mara nyingine huwa vigumu kwa mwamuzi kuyatambua ndiyo maana wenzetu waliopiga hatua kisoka duniani wamkuja na Teknolojia ya Kumsaidia Mwamuzi, VAR.

Lakini licha ya uwapo wa VAR bado makosa hayaishi na baadhi  yamekuwa yakionekana. Kwenye Ligi Kuu Tanzania kwa sasa waamuzi wanaonekana wao kazi yao ni kuchezesha mechi tu na si nyingine. Waamuzi hawalindi afya za wachezaji kwa kuachia rafu za ovyo.

Waamuzi wa sasa wanakumbwa na matatizo, kwanza wanaanza kuwa na wasiwasi na mechi, au presha wanapochezesha kuliko wachezaji wenyewe wanaocheza jambo ambalo husababisha kuegemea upande mmoja.

Tunadhani pia wanashindwa kujiamini wao wenyewe kwa sababu wanazozijua, kwani mwamuzi anatakiwa kuchezesha kwa haki na sio kuchezesha kwa wasiwasi na kufumbia macho rafu zisizo na maana.

Ikumbukwe pia wachezaji wanapoona mwamuzi hawalindi, hawawezi kuwa huru kutoa burudani kwa mashabiki, matokeo yake soka linakuwa halina ladha na hatimaye kupoteza watazamani uwanjani, hivyo ni wakati sasa kwa TPLB kulitazama hili kwa jicho la ziada.