Mwaka 2022 matukio mengi mabaya yalijitokeza kwa upande wa wanafunzi na kuwafanya wazazi kuwa katika wakati mgumu wa kuchagua sehemu salama kwa ulinzi wa watoto wao.
Wazazi wengi wanakuwa na amani na kufanyakazi bila wasiwasi, watoto wao wanapokuwa shuleni kwa sababu wanajua ni sehemu salama.
Hata hivyo, matukio yaliyojitokeza kwa baadhi ya shule walimu kuwafanyia ukatili watoto hao waliopewa jukumu na wazazi la kuwalea na kuwafundisha ili waweze kutumiza ndoto za maisha yao, yamewavunja moyo wazazi wengi na wengine kuathirika kisaikolojia.
Mwaka huu 2023 uwe ni wa ulinzi kwa watoto wasiwe waathirika wa matukio hayo ya ukatili ambayo huwafanya baadhi yao kupata athari kisaikolojia.
Wazazi wasikubali kuwaacha watoto wao bila kuwafuatilia kila siku wanaporudi kutoka shule kwa kuwachunguza na kuongea nao ili waweze kuwapa taarifa kama wamefanyiwa vitendo vyovyote vibaya.
Mzazi anapokuwa karibu na mtoto ni rahisi kupata taarifa, lakini anapokuwa mbali na mtoto wake kwa kisingizio cha kazi, atakuja kugundua madhara akiwa amechelewa.
Kuna vitu vingi ambavyo mwanafunzi anahitaji kuwa navyo ili asiweze kuharibiwa ndoto yake ya kufikia malengo aliyojiwekea.
Wazazi wengine wanatamani watoto wao wangepata mahitaji yote ambayo mtoto anatakiwa kuwa nayo awapo shuleni, lakini anashindwa kumtimizia kwasababu ya hali ya kiuchumi.
Watoto wengine hawaelewi hali wanazopitia wazazi wao na wanapoona wenzao wametimiziwa mahitaji yao, wanakuwa na tamaa na kuingia kwenye mtego wa kushawishiwa na watu wasiokuwa na nia nzuri kwao na kuwakatisha masomo.
Juzi Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka, aliagiza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza waripoti shuleni hata kama hawana sare za shule.
Hatua hiyo ya Mkuu wa Mkoa ni ya kupongeza kwa sababu wanafunzi wengi wanapoteza fursa walizozipata kwasababu tu ya kukosa sare kutokana na wazazi wao kutokuwa na uwezo wa kuwanunulia.
Ni kweli watoto wanapokuwa na sare zinawatambulisha kuwa ni wanafunzi na vile vile kuleta usawa katika mavazi ili kusiwe na tofauti kati ya mwanafunzi mmoja na mwingine.
Hata hivyo, cha msingi ni elimu atakayopata mtoto anapofundishwa na walimu, bila kujali amevaa vazi la thamani ya kiasi gani.
Vile vile, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwaagiza wakuu wa wilaya kwa kushirikiana na wakurugenzi na maofisa elimu, kusimamia dhamira ya serikali ya kutoa elimu bila malipo kuanzia darasa la elimu ya awali, hadi kidato cha sita kwa kutembelea shule na kukagua fomu za kujiunga na shule na kujiridhisha hakuna michango ya ovyo.
Kadhalika Jeshi la Polisi limewataka madereva wanaoendesha mabasi ya shule wajisimamie badala ya kusimamiwa ili kuhakikisha usalama muda wote.









