Chama hicho katika mkutano wao uliofanyika jijini Arusha na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana, kilipendekeza serikali kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo ili kuondoa usumbufu, urasimu na upotevu wa mapato unaoendelea kujitokeza kutokana na wingi wa kodi na tozo zinazotokana na utalii, ambazo hukusanywa na Wizara ya Fedha na Mipango na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Chama hicho kilipendekeza Wizara ya Maliasili na Utalii, kusimamia yenyewe makusanyo yote ya tozo na kodi tofauti na ilivyo sasa, ambapo kuna wizara nyingine mbili zinakusanya.
Kilitoa mfano wa tozo wanazotozwa watalii wanapopita kwenye maeneo ya halmashauri za wilaya, wakati wakiwa njiani kwenda kutazama vivutio mbalimbali katika Hifadhi za Taifa.
Utaratibu huo wa mifumo ya ukusanyaji wa kodi na tozo, unaoendelea kufanywa na taasisi nyingi, umedaiwa kukwamisha na kuchelewesha utekelezaji wa mikakati ya serikali ya kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania.
Kwa kweli hoja zilizotolewa na chama hicho ni za msingi kama serikali inataka sekta ya utalii iendelee kukua na kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini bila kupata vikwazo hivyo vya kodi.
Lengo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuitangaza filamu ya Royal Tour, ni kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya utalii ili kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini na kuongeza mapato.
Kama kutakuwa na mkanganyiko huo wa tozo na kodi, kutarudisha nyuma juhudi zote zilizofanywa na Rais za kutangaza vivutio vya utalii.
Chama hicho kilimwomba Rais Samia na serikali yake kuhakikisha masuala yote ya tozo na kodi yanasimamiwa na wizara moja.
Kadhalika, chama kilipendekeza maslahi duni wanayopata waongoza watalii yafanyiwe kazi, wakiwamo wanaopandisha wageni Mlima Kilimanjaro, ambao kwa muda mrefu wamelalamikia malipo ya ujira wa Sh. 5,000 hadi Sh. 10,000 hakilingani na kazi wanayofanya.
Kwa zaidi ya miaka 10 imedaiwa maslahi ya wapagazi katika Mlima Kilimanjaro, hayajafanyiwa kazi, huku wakipendekeza kuongezwa hadi kufikia dola 15 za Marekani, sawa na Sh. 30,000 za Tanzania.
Kutokana na maslahi duni, asilimia kubwa ya waongoza watalii wanakata tamaa ya kuendelea kunufaika na matunda ya utalii na wamekuwa wagumu kutoa mchango wao katika kulinda na kuimarisha rasilimali za utalii wanakuwa wagumu wa kujitolea kukabiliana na majanga ya moto.
Jambo la kufurahisha, waziri mwenye dhamana katika sekta hiyo alisema amepokea mapendekezo yaliyotolewa na wadau wa sekta hiyo, likiwamo la nyongeza ya posho za waongoza watalii na wapagazi kwa siku.
Suala la tozo pia ataliwasilisha katika ngazi zinazohusika ili lifanyiwe kazi na ikiwezekana mwaka ujao wa fedha, lianze kusimamiwa na wizara moja.










