Agizo kuwapo matroni kwenye mabasi ya shule litekelezwe

12Jan 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Agizo kuwapo matroni kwenye mabasi ya shule litekelezwe

BAADA ya kutokea kwa matukio ya unyanyasaji unaodaiwa kufanywa na makonda na madereva kwa wanafunzi wanaosoma shule zinazotoa usafiri wa mabasi, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, alitoa agizo la wamiliki wa shule hizo kuweka matroni atakayewasimamia.

Matukio yaliyoripotiwa ni madai ya makonda na madereva kufanyia ukatili wa kingono baadhi ya wanafunzi wanapowarudisha nyumbani nyakati za jioni.

Kibaya zaidi, inadaiwa makonda hao na madereva  hufanya vitendo hivyo kwa kumchangia mtoto mmoja.

Ni matumaini yetu kuwa agizo hilo litatekelezwa na wamiliki wa shule zinazotoa huduma ya usafiri kwa wanafunzi hao ili kuwaepusha na unyanyasaji huo wanaofanyiwa huku wakitishwa watawaua kama watasema kwa wazazi wao.

Jukumu la kuwaangalia watoto ni la jamii na inapotokea wanafanyiwa vitendo vibaya ni lazima hatua zichukuliwe kwa kuadhibiwa waliohusika kufanya hivyo.

Jana wakati Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe, akitembelea shule kuangalia wanafunzi walioripoti, aliagiza shule binafsi zote kuweka mwangalizi wa kike (matron) katika kila gari la wanafunzi ili kuepusha wanafunzi kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji au ukatili wa kijinsia.

Alisema katika wilaya yake ya Kinondoni, shule zote za binafsi zenye mabasi wameweka matron na hayo ni maamuzi ya serikali ya wilaya na lengo ni kutengeneza mazingira mazuri kwa watoto kutopata athari za mashambulizi au unyanyasaji wa kijinsia.

Mkuu huyo alisema asingependa katika wilaya yake yaliyotokea mwaka jana yatokee mwaka huu na kwamba ameshaunda timu ikijumuisha madawati ya jinsia kutoka Jeshi la Polisi na Maofisa Ustawi wa Maendeleo ya Jamii kwa pamoja kupita shule zote kuhakikisha mabasi yote ya watoto yana matron kule ndani.

“Lengo letu tunataka kila mzazi anapokabidhi mtoto anajua yuko maeneo salama, tunataka maeneo ya shule zetu za watoto mpaka mabasi yanaendelea kuwa salama kwa watoto wetu. Hatutavumilia shule yoyote ambayo kwenye basi itaweka msaidizi wa kiume, tunataka kuepukana na mazingira hatarishi kwa watoto wetu.”

Hatua hiyo ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ni ya kupongeza ili kuwanusuru watoto wasiendelee kufanyiwa ukatili na kuchukia shule.

Wakuu wengine wa wilaya wanatakiwa kuvalia njuga suala hilo ili kukomesha kabisa matukio hayo yanayokwenda kinyume na maadili.

Katika kuonesha kuwatia moyo watoto waliofaulu kuingia kidato cha kwanza katika wilaya yake pamoja na walimu wao, Gondwe aliagiza wanafunzi wote waliofaulu kwenda sekondari kwenye wilaya yake ambao hawana sare, kuripoti shuleni na kuanza masomo kwa kuvaa sare walizotoka nazo shule ya msingi.

Alisema ni vyema wanafunzi hao wakatumia sare walizokuwa wakitumia shule za msingi kuliko kukosa masomo.

“Wazazi wote ambao watoto wao wanaingia kidato cha kwanza wasijali, hata kama watoto wao hawana sare za shule, wahakikishe wanaenda shuleni, hatutaangalia kwamba hana sare au nini. Hatuwezi kusubiri mtoto akose masomo, hata kama ana sare zake alizozitumia shule ya msingi aje tu hivyo hivyo na mambo yatakwenda taratibu akiendelea kutumia hizo sare za msingi,” alisema Gondwe.

“Haitakuwa jambo jema watoto wamefaulu halafu wanabaki nyumbani kwa sababu eti hawana sare za shule, hatutaki kuona mtoto yeyote anabaki nyumbani kwa sababu hiyo wakati analipiwa ada na Rais Samia Suluhu.