Hali hiyo imejitokeza baada ya Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Athumani Amasi, kutangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha pili na darasa la nne iliyofanyikia Oktoba/Novemba, mwaka jana.
Matukio ya wanafunzi kuandika matusi au kuchora picha badala ya majibu ya maswali wanayoulizwa kwenye mitihani hiyo ni dalili kuwa wapo darasani, lakini hakuna umakini kwenye masomo.
Vile vile, wazazi au walezi wanapaswa kufuatilia maendeleo ya masomo ya watoto wao kila siku kwa kuwauliza maswali ya walichofundishwa shuleni na kuangalia madaftari yao kujua kama wanaenda sawa na wanachofundishwa.
Katika matokeo hayo imebainika kuwa wanafunzi 279 wamefutiwa matokeo, kati yao 82 ni wa darasa la nne, na 213 ni wa kidato cha pili baada ya kufanya udanganyifu na 14 wa kidato cha pili kuandika matusi.
Baraza la Mitihani limeamua kufuta matokeo yote ya wanafunzi waliobainika kufanya udanganyifu na walioandika matusi katika upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili mwaka 2022.
Lawama zimeenda kwa baadhi ya wazazi na walezi wanaodaiwa kuwadanganya wanafunzi, watoto wao kwa mbinu tofauti ili wafaulu.
Wazazi hao wanatakiwa kuwaacha watoto wao wafanye mitihani kwa uwezo wao na kama wakiandaliwa vizuri, hakuna kitakachoshindikana, watafanya vizuri na kufaulu.
Tabia ya baadhi ya wazazi kuwanunulia mitihani watoto wao ili waweze kufaulu mitihani, haiwasaidii kwa kuwa mwanafunzi atajaza majibu na kufaulu, lakini akimaliza shule hakuna atakachoelewa.
Ni vyema mtoto aachwe ajisomee ili aelewe anachojifunza hata akitoka shule anakuwa na maarifa ya kile alichofundishwa na kukielewa.
Mitihani mingine wanayouziwa wanafunzi si ya kweli matokeo yake anapokutana na maswali ambayo hakuyatarajia anaishia kuchora picha na kuandika matusi kama ilivyobainika katika matokeo yaliyotangazwa jana.
Katika matokeo hayo, Darasa la Nne, wanafunzi 1,320,700 kati ya 1,592,235 wamefaulu kwa madaraja tofauti, huku wasichana wakiwa ni asilimia 84.76 na wavulana 81.03.
Idadi ya wanafunzi waliofanya vizuri inatia moyo na ingeweza kuongezeka kama wanafunzi wote wangezingatia walichofundishwa na kuacha kutegemea mitihani ya udanganyifu.
Kadhalika idadi ya wanafunzi wa kidato cha pili, 539,645 waliofaulu kati ya 633,537, imeonesha jinsi wanafunzi walivyoonyesha bidii katika masomo na wachache ambao hawakuwamo kwenye orodha hiyo, wangeweza kufanya vizuri kama wangezingatia walichofundishwa na walimu wao.
Uzingatiaji wa masomo kwa wanafunzi ni jambo muhimu sana, ndio maana serikali iliamua kufanya mitihani ya darasa la nne na kidato cha pili ili kuangalia kama wanafunzi wanakwenda na wanaelewa wanachofundishwa badala ya kumuacha aendelee mpaka darasa la saba na kutoka akiwa mtupu kichwani.
Mitihani ya majaribio ina umuhimu wake inamsaidia mtoto kujielewa, mzazi kumfahamu mtoto wake na mwalimu kujua upungufu alio nao mwanafunzi wake ili aweze kumsaidia afanye vizuri.









