Wanahabari 40 kati ya 80 walioomba kupatiwa viwanja na halmashauri hiyo kwa mkopo wamekopeshwa.
Tunasema hiyo ni hatua nzuri aliyoanza nayo Meya wa Manispaa Iringa na ni mfano wa kuiga katika kuimarisha ushirikiano kati ya wanahabari na ofisi yake.
Orodha ya majina ya waandishi waliobahatika kukopeshwa viwanja hivyo, imekabidhiwa rasmi kwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi Mkoa wa Iringa (IPC), Frank Leonard kwa hatua zaidi.
Kutimizwa kwa ahadi hiyo, kumekuja kutokana na waandishi hao kuomba kupatiwa viwanja vinavyotolewa na halmashauri hiyo kwa mkopo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Mei 2022.
Kutimizwa kwa ahadi hiyo kunatia matumaini kwa wengine ambao waliomba kukopeshwa viwanja ili waondokane na adha ya kukosa nyumba za kudumu na usumbufu wa kupanga na kudaiwa kodi huku wengine wakidhalilika wakati mishahara inapochelewa.
Waandishi wa habari wanafanya kazi kubwa ya kuelimisha kupitia kalamu zao na vile vile kuhabarisha na kuburudisha. Pia wanapitia mazingira magumu katika ukusanyaji habari hizo.
Kama wanakumbana na changamoto katika kazi zao na wanaporudi nyumbani wanakosa amani kwa sababu ya kero za wenye nyumba kudai kodi, hata umakini unakosekana wanapokuwa wanafanya kazi ya kukusanya habari.
Katika yaliyopitishwa na Mkutano Mkuu Maalum wa IPC ni pamoja na la kutengeneza mwongozo maalum wa utatuzi wa migogoro utakaotumiwa na klabu zote, yenye (maazimio) kaulimbiu ya kutoka kuzuri kwenda kuzuri zaidi (moving from Good to Great).
Meya huyo alifafanua kuwa idadi ya waandishi wa habari wanaohitaji viwanda ni kubwa, lakini kwa kuanzia wametoa viwanja 40 kulingana na uwezo uliopo na wataendelea kutoa kwa waliobaki kadiri ya fursa zinapotokea.
Hata hivyo, Meya alisema uwezo wa halmashauri kuwapatia waandishi wote viwanja bure haupo, lakini uwezo wa kusubiri kwa kipindi kirefu kwa kuzingatia vipato upo.
Suala la makazi ya kudumu kwa waandishi wa habari ni msingi sana kwa vile wengi wao wanaishi katika nyumba za kupanga zenye changamoto mbalimbali na kusababisha baadhi yao kushindwa kufanya kazi zao kwa weledi.
Waandishi wa habari kama walivyo wafanyakazi wa tasnia nyingine wana mahitaji mengi kutokana na kazi zao kufanya katika mazingira magumu.
Waandishi wa nchi zingine zilizoendelea, husaidiwa kupata kadi zinazowawezesha kununua vitu katika maduka makubwa hata kama mshahara ukichelewa, wana uhakika wa kuishi na kufanyakazi bila mawazo.
Kazi yoyote mtu anapofanya anatakiwa asiwe na mawazo wapi atapata chakula au pesa ya kulipa kodi, mbali na changamoto zingine za ada za watoto, ili aifanye kwa weledi na asipate kishawishi cha kupokea rushwa.
Baadhi ya wafanyakazi hujiingiza katika matatizo sio kwa kupenda, lakini ni kutokana na mazingira yanayomlazimu kufanya hivyo na kujikuta akiingia matatani.
Meya wa Iringa umeonyesha mfano na viongozi wengine waige kuisaidia tasnia ya habari iweze kufanya vizuri zaidi.









