Kusimama kwa ligi hiyo kunatokana na michuano hiyo kujumuisha timu tano kutoka Tanzania Bara ambazo ni Yanga, Azam FC, Namungo, Singida Big Stars na mabingwa watetezi wa kombe hilo, Simba.
Ligi hiyo pendwa zaidi kwa Afrika Mashariki, inakabiliwa na changamoto mbalimbali lakini kubwa imekuwa ni waamuzi kuchezesha kwa kushindwa kufuata sheria 17 za soka zinazoulinda mchezo huo duniani.
Hilo ni tatizo ambalo kwa sasa linaonekana kuwa sugu na kuonekana moja ya chanzo kikubwa cha kuliathiri soka letu kwa mashabiki kupungua viwanjani kila uchao hivyo kusababisha klabu kukosa mapato.
Pamoja na matatizo hayo, sasa waamuzi wanaonekana kushindwa kusimamia ipasavyo kanuni muhimu ya kulinda afya za wachezaji uwanjani jambo ambalo ni hatari zaidi.
Soka la Tanzania hususan Ligi Kuu, waamuzi wamekuwa chanzo kikubwa cha wachezaji kucheza rafu mbaya kutokana na kuwa wagumu kuwaonya kwa kadi pale inapostahili.
Mfano mzuri ni katika mechi ya Kagera Sugar dhidi ya Simba iliyopigwa Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, tulishuhudia mshambuliaji wa 'Wekundu wa Msimbazi', Moses Phiri, akifanyiwa madhambi zaidi ya mara tatu bila mchezaji husika kuonywa kwa kadi ya njano hadi alipochezewa rafu mbaya zaidi na beki Abdulaziz Makame, hivyo kulazimika kutolewa nje kwa machela na vipimo vikionyesha atalazimika kukaa nje kwa zaidi ya wiki tatu.
Kama hiyo haitoshi, beki wa Simba, Henock Inonga, katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Benjamin Mkapa wiki iliyopita, alifanyiwa madhambi zaidi ya mara tatu, kabla ya mshambuliaji wa Prisons, Samson Mbangula, kumchezea rafu mbaya zaidi iliyomlazimu kutolewa kwa machela baada ya kushindwa kuendelea na mchezo, hivyo naye kuungana na Phiri katika chumba cha majeruhi.
Hakika ni rafu mbaya zimekuwa zikifanywa na wachezaji mbalimbali katika ligi hiyo ambazo hazihitaji kuvumiliwa na mwamuzi yeyote mwenye taaluma hiyo, lakini kwa namna wanavyoshindwa kuchukua hatua mara moja uwanjani, kunatutia mashaka kuhusu taaluma yao katika kazi hiyo.
Rafu ambayo inastahili kadi ya njano, unakuta mchezaji anaonywa kwa mdomo huku inayostahili nyekundu mara nyingine wakionywa kwa njano, hivyo kuwafanya wanaotenda makosa husika kuyaona ya kawaida.
Tunaamini kama mchezaji amefanya madhambi yanayostahili kadi ya njano akionyeshwa, itamfanya kucheza kwa tahadhari kuepuka kuigharimu timu yake, lakini asipoadhibiwa anaona kosa alilolifanya ni la kawaida, hivyo kuendelea na mchezo mchafu dhidi ya wapinzani wao.
Lakini, hili la afya za wachezaji linapaswa kuanzia kwa wachezaji wenyewe kwa kila mmoja kufahamu soka ndiyo ajira yao, hivyo kuhatarisha afya ya mwenzako ni kumuharibia maisha yake na familia, hilo likifanyika litaliheshimisha soka letu na kuongeza mvuto kwa mashabiki.
Katika kipindi hiki ligi hiyo ikiwa mapumzikoni, ni wakati muafaka kwa Chama cha Waamuzi (FRAT), pamoja na Bodi ya Ligi (TPLB), kushirikiana kutoa semina zaidi kwa waamuzi ili ligi hiyo itakaporejea kanuni na sheria 17 za soka ziweze kuzingatiwa ipasavyo.










