Matukio ya kujiua, kuua yanaweza kudhibitiwa

30Dec 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Matukio ya kujiua, kuua yanaweza kudhibitiwa

MATUKIO ya watu kujiua au kuua wenzao yanaweza kudhibitiwa kama watafuata ushauri wa madaktari na wanasaikolojia.

Mengi ya matukio hayo yanaeleweka, husababishwa na hasira na mihemko ambayo kama itadhibitiwa mapema itapunguza madhara.

Elimu kwa jamii ni jambo muhimu kwa sababu itawafanya watu kuelewa vitu vya kuepuka wanapoona viashiria vyovyote vya vitendo vya mauaji.

Imeshauriwa pia watu wanapohisi hali isiyo ya kawaida kuondoka eneo ama mazingira yanayochochea kutenda mambo mabaya. Njia hiyo imetajwa kuwa dawa inayoweza kudhibiti ama kupunguza matukio ya watu kujiua au kuua.

Daktari Bingwa wa Binadamu, Idara ya Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Rufani ya Kanda Mbeya, Raymond Mgeni, anaeleza kuwa jamii inapaswa kudhibiti msukumo wa hasira unaochochewa na sababu yoyote, ikiwamo kuudhiwa ama kusingiziwa jambo lolote kwa sababu ni kati ya visababishi vya ongezeko la matukio ya mauaji nchini ni ukosefu wa kudhibiti hali hiyo.

Takwimu zilizotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) mwaka juzi kuhusu haki za binadamu, zinaonesha kuwa watu wanne kati ya 10 waliojiua mwaka jana (2021), walikuwa ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35.

Ili kudhibiti matukio ya watu kujiua au kuua, jamii inapaswa ijenge mazoea na utaratibu wa kujifunza na kuwafundisha watoto. Kutoruhusu kuchukua hatua wapatwapo na msukumo huo na kuondoka eneo ama mazingira yanayowasababishia hasira.

Daktari anafafanua kuwa, matukio yanayoongezeka ya watu kujiua hutokana na kuchochewa na misukumo isiyodhibitiwa kutokana na hasira; ikiwamo mazingira yanayowazunguka na kusababisha mtu kuamua jambo bila kutarajia na kufahamu athari zake baadaye.

“Kuna wakati mwingine unaongea na mtu anakuudhi, kuna wengine hawana udhibiti, wengine wanaoudhiwa wanapoambiwa jambo ambalo hawajalitenda wanajikuta wakipatwa na hasira. Mwingine akipandwa na hasira anaweza kuchukua kitu ajichome au anywe sumu.”

Hali hiyo pia inaweza kuchangia kisasi na matukio mengi. Watu walikuwa kwenye mazungumzo wakapishana kauli mmoja ananyanyua jiwe au chupa na kumrushia mwenzake. “Tuidhibiti hali hiyo na iwe ni utaratibu kwenye maisha yetu ya kila siku.”

Ripoti ya LHRC kuhusu haki za binadamu kwa mwaka 2021/22, inazungumzia haki ya kuishi inavyokiukwa kutokana matukio kadhaa hasa ongezeko la mauaji yatokanayo na wivu wa kimapenzi.

Ripoti hiyo inasema, wanawake ndiyo waathiriwa wakuu wa matukio ya ukatili wa kijinsia, wanauawa na wapenzi wao kwa sababu ya wivu wa mapenzi, ingawa takwimu zinabainisha pia wanaume ambao wanaongoza kwa kuchukua maamuzi magumu ya kujiua.

Kadhalika, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonesha kwamba Watanzania milioni saba, wana tatizo la afya ya akili wengi wao wakiishi Dar es Salaam.

Pia kuna mtu mmoja hufariki dunia katika kila sekunde 40 kutokana na kujiua.

Aidha, takwimu za LHRC kuhusu haki za binadamu mwaka 2021, inabainisha kwamba watu wanne kati ya 10 waliojiua mwaka jana (2021) walikuwa ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35.