Vitendo vinatakiwa zaidi sasa kukomesha utapeli mtandaoni

03Feb 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Vitendo vinatakiwa zaidi sasa kukomesha utapeli mtandaoni

KWA muda mrefu kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kuongezeka kwa wimbi la watu wanaotumia mitandao ya simu za mkononi kufanya utapeli ikiwamo kuibiwa fedha au kutumiwa ujumbe mbalimbali ukiwamo wa vitisho.

Baadhi ya watu hao wanaotumia mitandao, wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali ikiwamo kuwaambia wananchi kwamba wamepokea fedha kimakosa, hivyo wafuate maelekezo wanayopewa ili kurejesha kurejesha miamala inayodaiwa kukosewa. Matokeo yake, baadhi ya watu wameibiwa fedha zao bila kujitambua na wanapofuatilia kwenye kampuni za simu husika, wanaambiwa kuwa miamala hiyo haitambuliki.

Aidha, baadhi ya watumiaji wa simu za mkononi, wamekuwa wakitumiwa ujumbe kwamba watoto wao walioko shule za bweni wanaumwa na wamelazwa hospitalini, hivyo wanatakiwa kutuma fedha kwa ajili ya matibabu. Kutokana na baadhi yao kuamini kwamba inawezekana watoto wao wanaumwa, hulazimika kutuma fedha na wanapokuja kushtuka, wanajikuta wameibiwa fedha zao.

Kwa jumla, kila uchao matapeli hao wamekuwa wakibuni mbinu mbalimbali zinazofanikisha azma zao za kuwaibia wananchi. Miongoni mwa mbinu hizo ni kutakiwa kulipa fedha kwa njia ya simu kwa kutumia namba fulani na kutuma fedha kiasi fulani kama wanavyoelekezwa ili kujiunga na Freemason.

Kama vile haitoshi, watu wameanza kupokea simu kwamba mganga wa kienyeji aliyeko sehemu fulani ni mtaalamu wa kumpa mtu utajiri, dawa ya mvuto kwa mchumba na kadhalika.

Kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo vya utapeli ambavyo vimewaingiza watu wengi mkenge, juzi, Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Nape Nnauye, aliibuka na kusema dawa ya watu hao inachemka na watashughulikiwa wakati wowote.

Waziri Nape ametoa kauli hiyo ikitoa matumaini kwa mara nyingine kwamba sasa watu wanaotumia mitandao kujitajirisha na wakati huo huo kuwaumiza wengine, sasa ujanja wao umejulikana na watakiona cha mtema kuni.

Pamoja na kauli hiyo yenye kutia matumaini, si mara ya kwanza kwa Watanzania kusikia jambo hilo kwa kuwa limekuwa likisemwa mara kwa mara na viongozi wa ngazi mbalimbali waliopewa dhamana ya kusimamia sekta ya mawasiliano. Licha ya kutoa kauli hizo na kwamba mwisho wa watu hao umefika, vitendo hivyo bado vinaendelea kuota mizizi.

Kwa mantiki hiyo, kutokana na hali iliyofikia kwa vitendo hivyo, itoshe kusema kwamba maneno yameshindwa na sasa vitendo vitumike, ikiwa na maana kwamba serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iwachukulie watu hao hatua kwa mujibu wa sheria badala ya kuendelea kutoa kauli tamu ambazo katu hazisaidii.

Tunasema hivyo kwa sababu watu hao namba zao zimesajiliwa kwa mfumo wa kielektroniki, hivyo wanajulikana kwa majina yao na namba zao za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Kwa mantiki hiyo, ni rahisi kuwapata na kuwachukulia hatua kama nia thabiti ya kufanya hivyo itakuwapo.

Ni dhahiri kwamba kama TCRA, na kampuni zinazotoa huduma za simu za mkononi na jeshi la Polisi watashirikiana kwa dhati, jambo hilo linaweza kufanyiwa kazi na kukomeshwa mara moja. Ni muda wa vitendo sasa maneno yawekwe kando.