Kuheshimu mikataba, silaha kuvutia wadhamini wengine

04Feb 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kuheshimu mikataba, silaha kuvutia wadhamini wengine

MIAKA ya nyuma klabu pamoja na vyama vya michezo ikiwamo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), vilikuwa na kilio cha kukosa wadhamini kwa ajili ya kuendesha mashindano yao mbalimbali.

Kila kukicha viongozi wa klabu pamoja na vyama vya michezo hapa nchini walilazimika 'kuombaomba' au msemo maarufu 'kutembeza bakuli' ili kupata fedha za kuendesha ligi zake pamoja na mashindano mengino waliyoyandaa kwa mujibu wa kalenda zao.

Wakati mwingine timu zilikuwa zinakwama hadi kusafiri kwenda katika vituoni au nje ya nchi kupeperusha bendera ya taifa kutokana na kukosa fedha za kugharamia tiketi na pengine kulipa ada ya ushiriki.

Hali hiyo ilizifanya klabu na vyama hivyo mara kwa mara kuyalilia makampuni na taasisi mbalimbali ili zijitokeze kuwekeza kwenye michezo yao ambayo mwisho wa siku ilitoa wawakilishi wa nchi kwenda kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Lakini katika kipindi cha miaka 10 sasa tumeshuhudia makapuni na taasisi mbalimbali zikijitokeza kuingia mikataba ya kudhamini timu au mashirikisho na kubadili taswira ya michezo yetu kutoka kuonekana ya ridhaa na kuwa ya kulipwa.

Udhamini mnono uliopatikana ulisaidia kuboresha ligi na mashindano mbalimbali, lakini pia ulisaidia kuwavutia na kuzipa klabu uwezo wa kusajili wachezaji wa kigeni ambao walisaidia kuongeza nguvu kwenye vikosi vyao na hatimaye timu za Tanzania kuanza kuogopeka.

Timu pia zilipata nguvu ya kuajiri makocha wa kigeni , lakini pia kufanya uamuzi wa kwenda kuweka kambi ughaibuni ili kufanya maandalizi ya kujiandaa na msimu mpya, timu zimenunua vifaa vya kisasa, zimetekeleza programu zake mbalimbali za kiufundi kutokana na fedha walizopata kutoka kwa wadhamini hao.

Ushindani katika ligi mbalimbali uliongezeka kutokana na zawadi nono ambazo sasa hutolewa lakini pia posho za ushindi wa kila mechi, ziliongeza ushindani ambao mbali za kuzipa timu matokeo chanya, wachezaji wa Kitanzania waliimarika na kutoa mchango mzuri pale walipoitwa kwenye Timu za Taifa.

Pamoja na mazuri hayo, inashangaza kuona siku za hivi karibuni klabu zimeanza kuvunja makubaliano na wadhamini wao, pengine kwa kudhamiria au kwa kujiona wao ni 'wakubwa' na kampuni hizo hazitawachukulia hatua.

Katika dunia ya sasa ukiona kiongozi anashiriki kuvunja au kukiuka makubaliano yaliyosainiwa, basi huyo haitakii mema taasisi ambayo anaiongoza, kwa sababu ikumbukwe imewachukua muda mrefu mabosi wa makampuni kuwekeza kwenye michezo kwa sababu ya baadhi ya viongozi kujichukulia maamuzi kwa kutoangalia madhara ya baadaye.

Kwa faida ya maendeleo ya michezo hapa nchini, ni vyema viongozi wa Yanga wakakaa upya na kujadiliana kuhusiana na malalamiko ambayo wamepewa na wadhamini wao wakuu, Kampuni ya Kubashiri Michezo ya SportPesa.

Ni wazi vikao vya pamoja vinaweza kulimaliza sakata hili ambalo limeonekana kuchafua 'hali ya hewa' wakati Yanga ikibakiza siku chake kuanza kuiwakilisha nchi na bendera ya klabu yake katika mechi za hatua ya makundi ya michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Tunaamini Yanga na SportPesa bado wana nafasi ya kukaa pamoja na kulimaliza  sakata hili na kuifanya 'ndoa' ambayo waliifunga inayotarajiwa kumalizika ifikapo mwaka 2025, ikaendelea kwa amani.

Kuendelea kukiuka mkataba, kunaweza kuigharimu Yanga kama ambavyo Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ilivyowahi kujiondoka kudhamini Ligi baada ya viongozi waliokuwa madarakani wakati huo TFF ikiitwa FAT kuongeza idadi ya timu kinyume na makubaliano.

Ikumbukwe SportPesa pia ni wadhamini wa timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ambazo ni Namungo FC ya Lindi na Singida Big Stars yenye makazi yake mkoani Singida na vile vile hutoa misaada mbalimbali kwa jamii, kitendo cha kuingia katika 'mzozo' na Yanga kinaweza kuathiri shughuli zake na pengine watakaoumia zaidi wakawa ni wadau wa soka hapa nchini.