Ligi Bara nafasi ya 5 ubora Afrika, waamuzi bado tatizo

06Feb 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ligi Bara nafasi ya 5 ubora Afrika, waamuzi bado tatizo

SHIRIKISHO la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS) limeitangaza Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa ya tano kwa ubora barani Afrika na ya 39 duniani kwa mwaka 2022, ikipanda kutoka nafasi 10 Afrika na ya 62 duniani, nafasi iliyokuwapo mwaka mmoja kabla.

Tuna kila sababu ya kulipongeza Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kwa usimamizi mzuri na kutengeneza mazingira safi na rafiki kwenye ligi hiyo hadi kuisaidia kupaa na kuzifunika ligi kubwa kama za Afrika Kusini, Zambia, Angola na Tunisia.

Japo kwa wengi inakuwa vigumu kuamini ni kweli Ligi Kuu Tanzania Bara imestahili nafasi hiyo, lakini ni wazi vipo vigezo vingi vimezingatiwa na IFFHS kabla ya kuona Tanzania inastahili nafasi hiyo kwa sasa, hivyo tukubaliane na waliofanya utafiti na wenye kupinga wapinge kwa utafiti.

Katika hilo ni wazi kitendo tu cha Ligi Kuu Bara kuvutia wachezaji wengi wa kigeni kuja kucheza soka hapa nchini hususani Afrika Magharibi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiamini maisha bora ya soka yapo Ulaya na Afrika Kaskazini maarufu nchi za Kiarabu, ni jambo la kuamini kwamba kweli ligi yetu inakua na inaendelea kupiga hatua.

Pia, awali ilikuwa wachezaji wakigeni wakija kucheza soka nchini, wengi watakuwa wa ukanda huu huu wa Afrika Mashariki na Kati na wakitua kuzichezea Simba ama Yanga tu, kitu ambacho kwa sasa ni tofauti kabisa kwani wametapakaa katika kila zote na ndio maana tunaona Wabrazil wenye viwango bora wakiitumikia klabu kama Singida Big Stars.

Lakini mafanikio ya Klabu ya Simba kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya kimataifa mara tatu, na kuiwezesha Tanzania kuingiza timu nne kwenye michuano ya Shirikisho barani Afrika (CAF), na msimu huu timu mbili zikitinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, Simba na Yanga ni mambo ambayo yalizoeleka kwa nchi za Magharibi mwa Afrika na Kaskazini.

Hivyo, pamoja na mafanikio hayo yote na mengine, bado TFF na TPLB, zina kazi ya kufanya ili kuendana na kasi hiyo ya soka letu kukua, hususan kumulika zaidi changamoto ya waamuzi ambao wanaonekana kuwa gonjwa sugu katika ukuaji wa mpira wetu.

Hii ni kutokana na kushuhudia kila uchao waamuzi wengi wakifungiwa, na hawa ndiyo ambao mashabiki wengi wanadai kusababisha soka la Tanzania kudumaa na kupoteza mvuto na wao kupoteza matamanio ya hudhuria uwanjani lakini kuwa kikwazo kwa wawekezaji kuongezeka.

Ni wazi ni vigumu kwa wawekezaji kujitokeza kuweka fedha zao katika mchezo ambao mtu mmoja tu anaweza kuamua matokeo ya timu kushinda ama kupoteza kwa kufinyanga sheria 17 za soka duniani, hivyo sekta hiyo inahitaji maboresho makubwa zaidi ili soka la Tanzania kuweza kupiga hatua.

Tunaamini kama TFF na TPLB kwa kushirikiana na Chama cha Waamuzi nchini (FRAT), wakielekeza nguvu zao katika kuzalisha waamuzi wengi na bora huku wakiboresha maslahi yao, ligi yetu itawashangaza wengi kwa kwa kupiga hatua zaidi na kuwavutia wachezaji wakubwa na wawekezaji.

Suala la ubovu wa waamuzi hili halihitaji mjadala, lipo wazi na ndiyo maana ni nadra kuona waamuzi kutoka Tanzania wakichaguliwa kwenda kuchezesha michuano yoyote mikubwa ya CAF, kama ilivyo kwa wenzetu wa Afrika Mashariki na Kati, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda ambao wamekuwa wakipata nafasi hizo mara kwa mara tena kwa idadi kubwa.

Tunatamani kuona kikifika kipindi kwa waamuzi wenyewe kujitathmini na kurejea sheria na kanuni zinazowaongoza katika kazi yao ili kulinda heshima na kumulika maslahi makubwa zaidi wakilenga fursa ya kuchezesha mechi kubwa na si za CAF tu bali hata za Fifa.

Kwa Ligi ya Tanzania kutangazwa kuwa nafasi ya tano kwa ubora Afrika na ya 39 duniani, ni aibu kubwa kuona waamuzi wake wakikosa nafasi ya kwenda kuchezesha mashindano makubwa yanayoandaliwa na CAF na Fifa na badala yake nchi kama Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda ambazo tumezipita kwa nafasi kubwa wenyewe waamuzi wao wakipewa nafasi hizo.