Hili la ajali, kila mmoja sasa awajibike kwa nafasi yake

07Feb 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hili la ajali, kila mmoja sasa awajibike kwa nafasi yake

NI kila wakati umma haupumziki, simulizi za kuumiza, ajali kila wakati.

Kwa mpito wa wikiendi hii simanzi zinatawala mkoani Tanga, hata kitaifa wanafamilia waliokuwa safarini kumpumzisha mpendwa wao mkoani Kilimanjaro, wakitokea Dar es Salaam, nao yamewakuta kwa pamoja.

Kinachoumiza sana ni pale wanandugu hao waliokuwa wanamsindikiza mzee wao wakampumzishe, nao wakaangukia wasifu huo wa kuitwa marehemu; wote wana unasaba wa karibu sana.

Unapowauliza wenye dhamana kuu wa Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani, maarufu kwa jina la Trafiki, nao wana malalamiko yao kuhusiana na hizo ajali zinavyowaweka kuwajibika na ulingo huo wa huzuni.

Wanakadiria asilimia 75 za ajali nchini zinatokana na uzembe wa madereva barabarani. Taarifa ya awali ni hata kilichojiri kwa wapendwa wa Tanga na baadhi yao waliwekwa kwenye nyumba ya milele, huko wilayani Rombo, Kilimanjaro jana, kisa ni nidhamu ya udereva.

Hasara ya ajali hizo ni zaidi ya madhara binafsi kiafya kwa wahusika ikiwamo ulemavu wa kudumu na mengine. Hapo hapo watu hao wanahudumiwa, hata kuangukia gharama kubwa maradufu.

Upo wakati mhusika anagharamia, pia anapokosa wa kumgharamia, hospitali husika hubeba mzigo kwa sura pana. Kama ilivyo kawaida ya matibabu hospitali nyingi na hasa za umma, huwajibika na kumhudumia mgonjwa kwanza na suala la malipo huwa linafuata.

Maana yake ni kwamba, hospitali inakuwa sehemu ya dhamana kumhudumia mgonjwa atakapokwama gharama, awe hai au inapotokea katangulia mbele ya haki.

Ni hivi karibuni tulifahamishwa kwamba ili kufanyia uchunguzi mwili wa aliyefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), inagharimu Sh. 250,000 kwa kila mwili.

Sasa katika mikasa ya vifo pale hospitali inapatiwa miili mingi ya kufanyia uchunguzi wa kutolea ripoti na pale haitagunduliwa ndugu na jamaa, dhamana ya gharama inabaki kwa mamlaka ya hospitali.

Kwa ujumla kuna hali ya kwamba kule barabarani kuna shida inayobeba sura zote, nidhamu na uwezo mdogo wa kumudu njia.

Tunajua kuna mengi sana yamefanyika kukabili hali hiyo kwa muda sasa, hata mamlaka husika na hasa polisi trafiki wako katika wakati mgumu.

Ulianzishwa utaratibu wa mafunzo kwa madereva katika Vyuo vya Elimu ya Ufundi (VETA) nchini, pia Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dar es Salaam, madereva wananolewa, lakini bado ni mtihani, ajali mbaya tunazidi kuzisikia.

Tuseme kuanzia usimamizi wa juu kiserikali, wakala wao barabarani polisi, madereva, abiria, wapitanjia na kila mtu anawajibika kwa maana hakuna hata mmoja aliye salama na ajali barabarani, kwamba haimgusi.

Ni kila mtu kwa nafasi yake anafaa kuchangia kukabili haya yanayotuondolea uhai kwa mpigo, kama kilichotokea mkoani Tanga mwishoni mwa wiki.