Bunge lisifanywe sehemu ya mipasho, na kuibua utengano  

10Feb 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Bunge lisifanywe sehemu ya mipasho, na kuibua utengano  

MKUTANO wa 10 wa Bunge unatarajiwa kumalizika leo jijini Dodoma baada ya kufanyika kwa takriban wiki mbili.

Katika mkutano huo, kuna mambo mengi yaliyofanyika yakiwamo maswali ya kawaida, maswali kwa Waziri Mkuu na taarifa za kamati za kudumu za bunge.

Baadhi ya taarifa za kamati hususan ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa, yaliibuliwa madudu yaliyofanywa na baadhi ya halmashauri hali iliyoonyesha kuwa bado kuna ubadhirifu na ufisadi wa kutisha katika mamlaka hizo zilizopewa jukumu la kutekeleza moja kwa moja miradi ya maendeleo ya sekta mbalimbali zikiwamo elimu, afya, maji, kilimo na miundombinu. 

Hatua hiyo imesababisha baadhi ya wabunge kuja juu na kuchukua hatua dhidi ya waliohusika ikiwamo kuchukuliwa hatua za kisheria badala ya kuwahamisha kutoka halmashauri moja kwenda nyingine, jambo ambalo limezoeleka. Kuwapo kwa madudu hayo si jambo geni kwani kila kamati zinapowasilisha ripoti zao, yamekuwa yakianikwa sambamba na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Pamoja na hayo ambayo ni kawaida kutokea kila mara, jambo kubwa ambalo limeibua mijadala ni kauli za baadhi ya wabunge na mawaziri walizozitoa wakati wa kuchangia taarifa mbalimbali na kujibu hoja zilizotolewa wakati wa mijadala. Moja ya mambo hayo ni kauli ya mbunge mmoja kulalamikia mfumo wa ajira katika utumishi wa umma na taasisi za serikali kuwa si rafiki, hivyo kushauri kwamba utaratibu wa sasa ubadilishwe na badala yake ufanyike kikanda!

Mbunge huyo bila kutafakari nini anachokisema na kwa mustakabali wa maslahi mapana ya taifa, alisema serikali itoe ajira kwa kigezo cha wilaya, mikoa au majimbo, ili vijana walioko katika maeneo hayo wanufaike!

Mtunga sheria huyo alikwenda mbali zaidi kwa kusema  baadhi ya vijana hasa wanaokaa vijijini kwenye wilaya na majimbo hutumia gharama za usafiri kwenda kwenye usaili wa kazi zinazotangazwa lakini wanazikosa, hivyo ni vyema ukaanzishwa mfumo wa kutoa nafasi kiwilaya na kimajimbo.

Licha ya kauli hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, alikabwa koo na baadhi ya wabunge pale aliposema watu waache kujadili masuala ya uchumi ambayo ni taaluma yake badala yake wakajadili masuala ya uganga wa kienyeji.  Hata hivyo, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, jana alitoa ufafanuzi baada ya kuombwa mwongozo na baadhi ya wabunge na kuona majibu hayo ya Waziri hayakuwa ya staha, hivyo kuyafuta katika kumbukumbu rasmi za bunge.

Wabunge ni watu wenye hadhi ya hali ya juu na jamii inaamini kwamba kwa kupata nafasi hiyo, wanapaswa kuzingatia miiko na maadili pamoja na tunu za taifa ambazo pamoja na mambo mengine ni uhuru, umoja na mshikamano. Kwa mantiki hiyo, wananchi hawatarajii kusikia habari za utengano na kubaguana kwa misingi ya udini, ukanda na ukabila, hivyo wabunge kwa kauli na matendo yao hawana budi kutambua hilo.

Jambo la kujiuliza ni je, kuna ulazima mtu mwenye heshima kama mbunge akasimama na kuhubiri habari za umajimbo kwa madai kwamba ajira kwa vijana katika serikali zitolewe kwa misingi hiyo? Kwa zaidi ya miaka 60 tangu nchi ipate uhuru bado kuna watu wanaendelea kuhubiri habari za umajimbo na umikoa kwa maana keki ya taifa igawanywe kwa misingi hiyo?

Hata majibu yaliyotolewa na waziri na hatimaye kuibua mijadala kila kona ikiwamo mitandao ya jamii, hayakuwa ya kistaarabu hata kidogo ndiyo maana Bunge limeamua kuyafuta kwenye kumbukumbu rasmi (Hansard).

Ni vyema wabunge, ambao ni wawakilishi wa wananchi, wakiwamo mawaziri, wakalitumia Bunge wakati wa mikutano yake, kuzungumza kauli zenye staha na kujiepusha na mambo ambayo yanaweza kuwa na sura na mitazamo ya kibaguzi. Kwa maneno mengine, Bunge lisifanywe kama kijiwe cha kujipatia umaarufu au mipasho.