Uwekezaji mkubwa unahitajika Simba, Yanga michuano CAF

20Feb 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Uwekezaji mkubwa unahitajika Simba, Yanga michuano CAF

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Simba na Yanga wameanza vibaya katika kinyang'anyiro cha Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho baada ya zote kupoteza ugenini kwenye mechi za awali za hatua ya makundi.

Simba ambayo inaiwakilisha Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, ilianza kwa kukubali kipigo cha bao 1-0 ugenini dhidi ya Horoya AC ya Guinea kabla ya kurejea nyumbani na juzi kuchapwa mabao 3-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco.

Matokeo hayo yanaifanya Simba sasa kubakiza michezo miwili nyumbani dhidi ya Horoya AC na Vipers ya Uganda huku ikiwa na mechi mbili pia ugenini dhidi ya Waganda hao na Raja Casablanca.

Watani zao, Yanga ambao wanaiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, wenyewe jana usiku walitarajia kuikaribisha TP Mazembe ya DR Congo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa ni baada ya kuchapwa mabao 2-0 ugenini dhidi ya US Monastir ya Tunisia katika mchezo wa awali.

Baada ya mechi ya jana usiku,  Yanga nayo inabakiza michezo miwili nyumbani dhidi ya US Monastir na Real Bamako ya Mali, wakati pia ikiwa na mingine idadi kama hiyo ugenini dhidi ya miamba hiyo ya Mali na TP Mazembe.

Kwa ujumla kwa viwango vilivyoonyeshwa na wawakilishi hao wa nchi, bila kujali matokeo ya mechi ya jana usiku kati ya Yanga na TP Mazembe, inaonyesha bado kunahitajika uwekezaji mkubwa husasan kwa upande wa usajili wa wachezaji wenye viwango vikubwa zaidi wanaoweza kuzipa matokeo chanya katika michuano hiyo.

Wachezaji wengi wanaosajili na timu zetu hususan Simba na Yanga, ni wale ambao tayari wameshindwa kufanya vizuri katika klabu kubwa za nje ambazo ndizo wanapambana nazo kwenye michuano hiyo ya CAF, jambo ambalo linazifanya kupata wakati ugumu wa kushinda kutokana na kuzidiwa ubora.

Tunatambua ni vigumu kwa klabu za Tanzania kuweza kuonyesha msuli katika vita vya kuwania kusajili wachezaji wazuri dhidi ya klabu kubwa za Kaskazini (Uarabuni), ambazo zina nguvu kubwa kiuchumi, lakini Nipashe tunaona bado inawezekana kupata wachezaji wazuri wanaoweza kutoa ushindani dhidi ya miamba hiyo kama zitawekeza katika wataalamu.

Tunaamini kinachozifelisha klabu zetu ni kukosa wataalamu wazuri katika idara zao za usajili, ambao wanatumia msimu mzima kufuatilia baadhi ya nyota wanaowahitaji kusajiliwa pindi dirisha la usajili linapofunguliwa.

Pamoja na timu za Kiarabu kuwa na nguvu kubwa kiuchumi, bado haziwezi kusajili wachezaji wote bora barani Afrika, hivyo kinachotakiwa kwa klabu zetu ni kuwekeza wataalamu zaidi katika idara zao za usajili na hapo zinaweza kupata wachezaji wenye vipaji ambao si tu watazisaidia kwenye michuano ya kimataifa kama hiyo, bali wataziingizia fedha nyingi kwa kuwauza hapo baadaye.

Mara nyingi, klabu za Tanzania husasan Simba na Yanga, hutegemea kumuona mchezaji katika mechi moja ama mbili tu alizoichezea klabu yake tena ilipocheza na moja kati ya hizo mbili na kuifunga, jambo ambalo si kipimo sahihi cha kutosha kumsajili mchezaji.

Hivyo, bila Simba, Yanga na klabu zingine za Tanzania kubadili mfumo wao mzima wa usajili, zitaendelea kuumia kila msimu kwa kushindwa kufika mbali kwenye michuano hiyo ya kimataifa yenye utajiri mkubwa na inayovutia mashabiki wengi kwenda uwanjani kuzishangilia.

Umefika wakati kwa Simba na Yanga na klabu zingine za Ligi Kuu, kuacha utamaduni wao wakusajili wachezaji walioonekana hawafai katika klabu kubwa, lakini pia kutosajili kwa sababu mchezaji husika ameifunga timu mojawapo kati ya hizo mbili.