Simba inayoipeperusha bendera ya nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, itakushuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kesho, Jumanne dhidi ya Vipers ya Uganda wakati Yanga yenye dhamana kama hiyo kwenye Kombe la Shirikisho barani humu, ikiikaribisha Real Bamako ya Mali uwanjani hapo Jumatano.
Hizi ni mechi za marudiano baada ya awali Simba kushinda ugenini bao 1-0, wakati watani zao, Yanga wakilazimisha sare ya bao 1-1 nchini Mali wiki moja iliyopita.
Katika Kundi C, ilipo Simba na pointi zake tatu, inashika nafasi ya tatu nyuma ya vinara Raja Casablaca ya Morocco yenye alama sita na Horoya ya Guinea iliyojikusanyia pointi nne, huku Vipers ikiburuza mkia kwa pointi yake moja.
Kwa upande wa Yanga ambayo ipo Kundi D ikiwa na pointi nne, hadi sasa inashika nafasi ya pili nyuma ya US Monastir ya Tunisia yenye alama saba huku TP Mazembe ya DR Congo ikiwa katika nafasi ya tatu na pointi tatu mbele ya Real Bamako yenye alama mbili mkiani.
Hivyo, katika makundi yote mawili ya wawakillishi hao wa Tanzania, lile la Simba na la Yanga, bado nafasi za kutinga robo fainali zipo wazi kwa kila timu, kinachotakiwa tu ni kila moja kuchanga karata zake vema kwenye mechi mbili mfululizo zijazo za nyumbani kabla ya kwenda kumalizia ugenini.
Kwa mujibu wa ratiba, inaonyesha kuwa rafiki zaidi kwa Simba na Yanga kwani baada ya mechi zao za Jumanne na Jumatano, timu hizo zitashuka tena Uwanja wa Benjamin Mkapa Machi 18 na 19, mwaka huu kuzikaribisha Horoya na US Monastir.
Tunatambua mashabiki hawataziangusha timu zao hususan zinapocheza katika Uwanja wa Mkapa, hivyo kilichobaki ni wachezaji kuelewa hizi si mechi za kucheza 'kirembo' wakimulika kushangiliwa na mashabiki jukwaani, kwani kinachotakiwa ni ushindi wa kishindo kwanza.
Hizi ni mechi za matokeo mbele hivyo kila mchezaji atakayepewa nafasi ya kucheza, anapaswa kutambua lengo ni moja tu, ushindi kwanza na kuweka mbwembwe nyingine kando.
Tunawasihi kutocheza na jukwaa kwani hakutusaidia timu wala mchezaji husika, hasa kwa kutambua ili malengo ya kila upande yatimie hawana budi kusonga mbele kwenye michuano hiyo na hilo si tu litaisaidia klabu, bali hata wachezaji watazidi kupata fursa ya kutangaza vipaji vyao kwa maslahi makubwa zaidi.
Tunaamini kwa idadi kubwa ya mashabiki ambao hujitokeza kutimiza nafasi yao kama mchezaji wa 12 uwanjani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa hususan katika mechi hizi za kimataifa, jukumu kubwa lililobaki ni wachezaji kucheza 'pira mchakamchaka' mwanzo mwisho ili kuwanyima pumzi wapinzani.
Ifahamike ushindi wa Simba kesho na Yanga keshokutwa, ndio utakaoleta morali ya kupambana zaidi katika mechi zijazo kwani utazidi kuzipa nafasi ya kufuzu robo fainali, hivyo ni wakati wa wachezaji kupambana kwa jasho na damu ili kuhakikisha wanapata matokeo katika mechi hizi za Jumanne na Jumatano.
Tunataka kuona Simba na Yanga, msimu huu zikiweka rekodi ya kufuzu hatua ya robo fainali kwa pamoja kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika na hilo litawezekana tu kama kila mchezaji, makocha, viongozi na mashabiki watatimiza wajibu wao, hivyo tunawatakiwa wawakilishi wetu hao kila kheri.









