Wafanyabiashara hiki ni kipindi cha kupata thawabu

24Mar 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wafanyabiashara hiki ni kipindi cha kupata thawabu

WAKATI Waislamu nchini wakianza mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan, viongozi mbali mbali wa serikali  na dini wamewataka wafanyabiashara kutopandisha bei za bidhaa hasa za vyakula ili kuwawezesha wafungaji kumudu kununua.

Rai hiyo ya viongozi hao inatokana na mazoea ya kila inapofika kipindi cha mfungo, wafanyabiashara kukitumia kama cha kupatia faida.

Bei za vyakula sokoni na madukani hupanda ghafla na kuwafanya wanaofunga kushindwa kumudu gharama za vyakula vya futari na kuishia kula ugali au wali.

Watu wanapofunga kutwa nzima na jioni wanapofungua vinywa wanatakiwa kuanza na vyakula laini kama inavyoshauriwa na wataalam wa afya kwa kuzingatia mlo unaotakiwa.

Vyakula vinavyopendwa wakati wa mfungo ni aina ya nafaka kama maharage, kunde, ngano na vile vyenye asili ya mizizi kama mihogo, magimbi na viazi vitamu na vingine vinavyopendwa kuliwa wakati huo.

Hata hivyo, inapofika kipindi hiki cha Ramadhani, bidhaa hizo ambazo hazionekani kwa wingi sokoni kipindi cha kawaida, huanza kuibuka na bei zake huwa hazishikiki.

Inavyoonekana baadhi ya wafanyabiashara huamua kuziweka pembeni wakisubiri kipindi hiki ambacho huhitajika kwa wingi na kuzimwaga sokoni kwa ajili ya kupata faida kubwa.

Vyakula ambavyo huonekana kwa wingi wakati wa mfungo ni maboga, mihogo na vile vinavyotokana na bidhaa zitokanazo na nafaka ya ngano.

Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, aliwaonya wafanyabiashara visiwani humo tabia ya kupandisha bei ya vyakula kipindi cha mfungo kwa kuwa hawawatendei haki wanaotafuta thawabu kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwafanya washindwe kununua bidhaa.

Mufti wa Tanzania, Shekhe Abubakar Zubeir, pia alikemea tabia hiyo na kuwaasa wafanyabiashara kuwa ni vema kipindi hiki cha mfungo wakawaonea huruma wale wanaofunga kwa kushinda na njaa na kuwafanyia wepesi wanapofungua ili wafanyabiashara hao wapate thawabu kwa Mwenyezi Mungu.

Kipindi hiki cha mfungo ambacho waumini wa dini za Kikristo (walioanza mfungo wiki tatu zilizopita) na Waislam walioanza jana ni cha kuomba toba kwa Mungu ili waweze kusamehewa dhambi zao.

Pia, kipindi hiki watu wengi hufanya mema kwa kuwakumbuka wenye shida kama za ugonjwa, wasiokuwa na uwezo kimaisha na wenye uhitaji kwa kuwapa misaada ili nao wanaposhukuru kwa misaada hiyo, watoaji wanapata baraka.

Kipindi hiki ambacho watu wanatakiwa kutenda matendo mema ni vema kila mtu akakitumia kufuta madhambi yake ya nyuma kwa kurudisha mema kwa Mwenyezi Mungu.

Vivo hivyo kwa wafanyabiashara wanatakiwa kutenda mema kwa kuwahurumia wenzao wanaofunga kwa kuuza bidhaa zao kwa bei halali na hata ikiwezekana wasiangalie kupata faida kubwa kwa kuwaumiza wanaonunua. Mungu huwalipa wanaotenda mema kwa njia nyingi.

Unaweza ukatenda jambo jema leo, lakini ukarudishiwa wema wako baadaye ukiwa umeshasahau kuwa ulimtendea mtu jambo jema.

Hivyo, kipindi hiki kitumike kwa watu wote kutenda mema ili kila mtu afurahie kufunga wakati akitubu kwa yale aliyoyatenda ambayo hayakumpendeza Mungu.

Mtu anapofunga huku moyoni akiwa na masikitiko au akiwaza atakula nini ni sawa na kushinda na njaa.

Tunawatakia mfungo mwema Waislam wote.