Adhabu wanazotoa walimu zichunguzwe

27Jan 2023
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Adhabu wanazotoa walimu zichunguzwe

SERIKALI ya Mkoa wa Kagera, imefikia uamuzi wa kumsimamisha kazi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kakanja ya mjini Bukoba,...

... baada ya kuonekana kwenye video fupi iliyokuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, akiwaadhibu wanafunzi wake kwa kuwachapa viboko kwenye nyayo zao huku akiwa amemkanyaga mmoja wao miguuni.

Uamuzi huo uliotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, tunasema unastahili kwa sababu kitendo alichokifanya mwalimu huyo ambaye ni mkuu wa shule kuwa ni cha kinyama.

Tunasema adhabu zinazochukuliwa kinyume na haki za binadamu ni lazima zichunguzwe ili kukomesha tabia hiyo inayofanywa na baadhi ya walimu.

Adhabu hizo zinaweza kuathiri watoto si kimwili tu hata kisaikolojia na kuwafanya wachukie shule na kusababisha kuwa na taifa la watoto wasiokuwa na elimu.

Unapompiga mtoto kwenye maeneo ambayo yanaweza kumletea ulemavu ni kwenda kinyume na haki za binadamu.

Kwa tukio hilo na mengine mengi yanayojitokeza kwenye baadhi ya shule kwa kutoa adhabu kali na zingine za udhalilishaji ni lazima hatua za haraka zichukuliwe kukomesha.

Kama kusingekuwa na mwalimu aliyechukua video hiyo na kuirusha kwenye mitandao ya kijamii, ina maana tukio hilo lingenyamaziwa na mwalimu huyo angeendelea kuathiri watoto wengine.

Kuna umuhimu wa kufanya uchunguzi hata kwa kuongea na watoto kujua madhila wanayopitia kutoka kwa walimu wao ili hatua zichukuliwe.

Tunaona hatua pia zimechukuliwa kwa walimu wengine wa Shule ya Msingi Kakanja, walionekana kufurahia adhabu aliyokuwa akitoa mwalimu mkuu kwa wanafunzi hao.

Hatua hizo ni kuhamishwa katika shule hiyo na kupelekwa sehemu nyingine. Lakini tunaona kuhamishwa sio suluhisho kwa sababu hata huko wanakokwenda wanaweza kuendeleza tabia hiyo.

Iliamriwa kuwa pamoja na mamlaka nyingine ikiwamo Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kuendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo, walimu hao hawapaswi kuendelea kuonekana katika maeneo ya shule hiyo na kuagiza wapelekwe walimu wengine wenye nidhamu nzuri waendelee na majukumu ya kuwafundisha watoto.

Pia madaraka ya Mratibu Elimu, Kata ya Kakanja, yamesitishwa tangu Januari 23, kwa kushindwa kutelekeza wajibu wake kama msimamizi wa elimu na nidhamu katika eneo lake na atapangiwa majukumu mengine.

Hili la watu kufanya makosa na kupangiwa majukumu mengine tunaona linawafanya watu kuwa na kiburi kwa sababu ya kujua kuwa watapewa kazi nyingine na kuendelea kupata mshahara.

Wanaofanya makosa hayo wanapaswa kupewa adhabu kali ili wajutie kile walichokifanya na pia iwe fundisho kwa wengine.

Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule lilipotokea tukio, alieleza wazi kuwa akiwa shuleni hapo alifika ofisini kuwasalimia walimu wenzake na kukuta malalamiko dhidi ya mwalimu mkuu huyo, kuhusu njia aliyoitumia kuadhibu watoto hao.

"Nilikwenda kumweleza mwalimu mkuu namna anavyolalamikiwa na walimu kutokana na njia aliyoitumia kuadhibu watoto hao, akaniambia amenielewa na hatarudia tena kitendo hicho, lakini akaniomba niende kumwombea radhi kwa walimu wenzake kwamba limetokea tu na hatarudia tena."

Mwalimu ni mlezi wa watoto anatakiwa kudhibiti hasira ili aweze kuwa mfano mzuri kwa anaowafundisha.