Mradi huo una lengo la kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi shoroba hizo kwa wanyama na wakazi wa maeneo husika ili nao wawe sehemu ya kulinda maeneo hayo ili waweze kuyatumia kwa muda mrefu na kurithisha vizazi vyao.
Kupitia mradi huo taasisi zinazojihusisha na uhifadhi zitapata fedha ya kuendesha miradi kuanzia Dola 200,000 (takribani Sh. bilioni 4.6) kwa mwaka na kama zikifanya vizuri zinaweza kuongezewa mkataba hadi miaka mitatu lengo likiwa ni kuzishirikisha katika uhifadhi huo.
Tunaamini juhudi zinazofanywa kupitia mradi huo, pamoja na juhudi za serikali, jamii na wadau wote wa uhifadhi zitaleta manufaa makubwa kwa serikali, wananchi na wazawa wanaoishi kwenye maeneo yenye shoroba hizo ambazo huchangia kukuza uchumi wao.
Baadhi ya faida wanazopata wakazi wanaoishi maeneo yenye shoroba hizo ni shughuli za utalii kutokana na wanyama wanaopita maeneo hayo, kilimo, pamoja na upatikanaji wa matunda, dawa na maua kutoka kwenye miti iliyoko katika hifadhi hizo.
Ni muhimu pia kuwapo na mipango shirikishi na wazawa katika kutafuta suluhu ya kutunza shoroba hizo ili kuwapo na suluhisho rafiki kwa pande zote mbili na jamii iwe sehemu ya kutunza maliasili hizo kwa kuwa vyanzo vikuu vya kutoweka kwake ni shughuli za kibinadamu na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Shughuli za binadamu kama vile kilimo, ujenzi wa nyumba za makazi katika mapitio hayo zinakuleta usumbufu kwa wanyama hao na kusababisha kuvamia makazi na huku kundi kubwa la binadamu likipata madhara na wanyama kutoweka.
Aidha, uamuzi wa kujikita pia kwenye kuboresha sera na miongozo ya uhifadhi na kutengeneza sera mpya nzuri kwenye maeneo ambayo hayana sera ni wa muhimu kwa sababu utachangia kuwapo na usimamizi mzuri katika maeneo hayo.
Katika ripoti ya Ofisi ya Makamu wa Rais ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira mwaka 2022-2032 inaonyesha takribani spishi 2,100 zipo hatarini kupotea ikiwamo mimea 895, wanyama 841 kama hakutokuwa na usimamizi mzuri katika hifadhi zetu na kusababisha baadhi kutoweka ikiwamo shoroba za wanyamapori.
Ripoti hiyo imetaja baaadhi ya shoroba zilizohatarini kuharibiwa na kuwa ni Wami-Mbiki (Hifadhi za Taifa za Saadani, Mikumi na Selous), Kwakuchinja-Mbugwe (Hifadhi ya Taifa ya Tarangire), Mayoka-Magara-Mwada-Vilimavitatu (Hifadhi ya Taifa ya Tarangire), Jangwani (Eneo la Pori la Mto wa Mbu) Kitete- Lositete ya Juu (Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro) na Laja (Hifadhi ya Ngorongoro na Msitu wa Marang).
Pamoja na kazi nzuri inayofanywa kupitia mradi huo, kama jamii iishio maeneo husika, serikali na wadau wa uhifadhi hawatokuwa na moyo wa kujitoa kusimama katika kuboresha hifadhi hizo itakuwa ni kutwanga maji kwenye kinu kwa kuwa hali ya shoroba itaendelea kuwa mbaya na hatimaye kupotea kabisa.









