Katika utaratibu huo viongozi wengine huwakaribisha wananchi ofisini kwake na mmoja mmoja huingia na kueleza kero au mapendekezo yatakayowarahishia kuongoza vizuri.
Baadhi yao huamua kufanya ziara kwa kuwatembelea wananchi walipo na kufanya mikutano ya hadhara na hapo hupewa nafasi ya kuuliza maswali au kutaja kero zinazowakabili.
Ziara hizo za viongozi huibua madudu mengi ambayo yalikuwa yamejificha kwa wale wanaoyoyafanya kujiamulia vyovyote wakijua hakuna anayewafuatilia.
Moja ya madudu yaliyoibuliwa katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, alipotembelea Wilaya ya Manyoni na kuwataka wananchi waeleze kero zao na ndipo aliposimama mwananchi mmoja na kulalamika kuwa baadhi ya madaktari wanakwenda kazini wakiwa wamelewa hali inayowatia hofu kwa usalama wa maisha yao.
Mwananchi huyo alilalamika kuwa alimpeleka mwanawe hospitali na kumkuta daktari akiwa amelewa chakali na kushindwa kuwahudumia.
Hali hiyo ya baadhi ya madaktari kufika kazini wakiwa wamekunywa pombe imedaiwa kujitokeza mara kwa mara katika hospitali yao na wananchi kuingiwa hofu ya usalama wa maisha yao.
Kwa kweli hiyo inatia hofu kwa sababu daktari anategemewa katika kumsaidia mgonjwa kujua tatizo lake na kumwandikia dawa ili aweze kupata tiba.
Kama daktari huyo anayetegemewa anafika kazini akiwa hajiwezi kwa kulewa na wagonjwa wakisubiri huduma yake hilo ni tatizo kubwa na halina budi kuchukuliwa hatua za haraka ili wananchi wasaidiwe kuondokana na kero hiyo.
Tabia ya baadhi ya watumishi kuingia kazini wakiwa wamekunywa pombe inapunguza ufanisi wa kazi na vilevile inahatarisha maisha, ustawi wa taasisi au kampuni anayofanyia kazi.
Miongoni mwa watu hao wanaaminiwa na viongozi wao kwa kupewa nafasi za juu, lakini wanashindwa kuonesha ufanisi na kuwaangusha wale waliowapendekeza kushika nafasi hizo.
Mara nyingi watu wa aina hiyo wanapokwenda kutafuta kazi wanakwenda kwa unyenyekevu, lakini wanapozipata wanasahau shida walizopitia na kuanza kuchezea nafasi walizozipata kwa kuingia kazini wakiwa wamechelewa huku wakiwa wamekunywa pombe.
Wengine hudiriki kuondoka kazini huku wakiwa na majukumu mezani mwao ya kufanya na kuchelewesha mipango mingine na kwenda kwenye shughuli nyingine zisizo za kiofisi.
Watu hao huwa wa kwanza kulalamika inapotokea kampuni au taasisi kutikisika kiuchumi na kuamua kupunguza wafanyakazi, akiwa kwenye orodha ya wanaotakiwa kuondoka.
Anasahau kuwa alipokuwa kazini alikuwa akifanya mambo ya ovyo na kutothamini kampuni yake inayomlipa mshahara kila mwezi ambao pengine alikuwa akiwazidi hata wenzake wanaofanyakazi kwa ufanisi na nidhamu.
Ndiyo maana kwa wale waliobahatika kutembelea nchi za wenzetu walioendelea, watu wanalipwa kutokana na kazi wanazofanya. Wengine hudiriki kufanya kazi zaidi ya moja ili aweze kupata kipato zaidi cha kumsaidia kuendesha maisha yake vizuri.
Wewe unayefanyakazi kwa kulipwa mshahara kila mwezi ambao haulingani na kazi unazozifanya ni sawa na kumwibia mwajiri wako kwa kuchukua malipo ambayo hukuyafanyia kazi.










