Moja ya jitihada za udhibiti ni kujenga ukuta eneo la Mererani mkoani Manyara, ili kuepusha uchepushaji wa madini aina ya tanzanite ambayo pekee hupatikana nchini, lakini biashara hiyo ilifanyika nchi jirani na kufifisha ukweli wa upatikanaji wa rasilimali hiyo.
Nyingine ni kujenga masoko ya madini kwenye mikoa mbalimbali hasa yenye uzalishaji wa rasilimali hiyo ambayo yameonyesha mafanikio makubwa ikiwamo halmashauri kupata kodi ya huduma.
Aidha, uwapo wa masoko hayo iliboresha bei ya madini na katika kila kilichouzwa kiliuzwa kwa njia halali na kuiwezesha nchi kupata mapato sahihi na kwa wakati tofauti na awali ambayo ilifanyika kwa kificho.
Mwaka 2017 Bunge lilifanya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ambayo iliongeza malipo ya mrabaha kutoka asilimia nne hadi sita kwa madini ya metali yakiwamo dhahabu, shaba na fedha. Pia, iliongeza malipo ya mrabaha kutoka asilimia tano hadi sita kwa madini ya vito yakiwamo rubi, garnets na tanzanite.
Mbinu nyingi za udhibiti zilifanyika kwenye marekebisho ya Sheria ya Fedha na Sheria ya Kodi ambayo inataka kila kampuni au mtu anayetaka kusafirisha madini nje ya nchi, madini yake yatakaguliwa na kuthaminishwa na atalipa ada ya ukaguzi ambayo ni asilimia moja ya thamani ya madini anayosafirisha.
Kutokana na sheria hiyo, mchimbaji mdogo anayeuza madini kwa wanunuzi wa kati au wanunuzi wakubwa atakatwa asilimia tano ya thamani ya madini na kupelekwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Pia kwenye mipaka kumekuwa na udhibiti kuhakikisha madini hayatoki kiholela nchini bali Watanzania wanaona manufaa kupitia kodi mbalimbali ambazo huingia kwenye kuhudumia huduma za kijamii.
Kauli ya Rais kuwa utoroshaji bado upo maana yake mamlaka zinazohusika hazijatekeleza wajibu wake sawasawa kusimamia na kulinda rasilimali hiyo isitoroshwe, hivyo kuathiri masoko yaliyojengwa, hivyo serikali kukosa mapato.
Tayari vyombo vya dola vimeagizwa kufuatilia kwa karibu ili kudhibiti wanaofanya hivyo, na tunatarajia kuona hatua zaidi zinachukuliwa na inawekwa wazi waliohusika na kilichofanyika kukomesha hali hiyo.
Ni lazima hatua zichukuliwe haraka ili kuepusha Tanzania kuwa shamba la bibi kwamba kila mtu anaweza kujichotea rasilimali awezavyo na kutoweka nazo pasipo kujulikana.
Bila udhibiti wa rasilimali hiyo nchi itaendelea kupoteza zaidi, hivyo ni lazima kukomesha mtandao wa utoroshaji ikiwamo kurudisha nguvu ya udhibiti iliyofanyika kipindi cha nyuma na kuwafikisha mahakamani wote wanaohusika ili iwe fundisho kwa wengine.
Kuacha mianya hiyo ni kuwakatisha tamaa wale wanaolipa kodi stahiki, huku wengine wakijinufaisha kwa njia za panya ambazo zinaumiza wengi.










