Alisema sekta ya Afya inachukua nafasi kubwa ya Wizara kuliko nyingine, na kwamba kama itatengwa na kubaki yenyewe usimamizi wa sera na sheria utakwenda vizuri, huku akisema atamshawishi Rais wa Zanzibar, kufanya hivyo hivyo.
Kwa mujibu wa Rais Samia, pamoja na jitihada nyingi zilizofanywa, mipango na sera bado nchi haijafika inapotakiwa kufika na ili kufikia lazima kuwe na usimamizi, uratibu, utathmini na ufuatiliaji wa sera na utekelezaji wa mipango wa afya na mambo mengine.
Tunapongeza uamuzi huu mzuri ambao umekuwa ni matamanio ya wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) zinazojihusisha na masuala ya wanawake na watoto, ambao waliona namna Wizara ya Afya ‘ilivyomeza’ idara nyingine kiasi cha kukosa nguvu.
Kuundwa kamati na kama pia itaundwa Wizara ya kushughulikia masuala hayo muhimu, ni matarajio yetu kuwa wadau wote muhimu watashirikishwa vyema kuhakikisha kuna mabadiliko makubwa.
Tunaamini kamati itafanya kazi nzuri ikiwamo kuzitazama sheria ambazo zinahitaji marekebisho, ikiwamo Sheria ya Ndoa, ambayo inakinzana kwenye umri wa kuoa na kuolewa.
Pia, tunaamini itafanyika tathmini ya kazi ya kamati hiyo kwa kupima matokeo chanya ambayo yametekelekezeka na kuisaidia jamii ya Watanzania.
Wanawake wanafikia asilimia 60 ya nguvu kazi ya kiuchumi na bado wanakabiliwa na vikwazo ikiwamo ustawi duni wa kiuchumi, kijamii na kisiasa na hakuna utekelezaji kama inavyotakiwa licha ya kwamba nusu ya watu duniani ni wanawake, hawajatumiwa vyema kuchangia maendeleo ya nchi.
Alisema Jukwaa la sasa la kizazi endelevu ni muhimu na kwamba hakuna anayeachwa nyuma na lengo namba tano la Malengo Endelevu ya Milenia (SGD) linatekelezwa, na kwa hesabu zilizopo duniani wanawake wanaweza kuchangia zaidi ya Dola za Marekani trilioni 28.
Kama ilivyo maeneo mengine duniani bado kuna vikwazo kwenye utekelezaji wa sera za kumuinua mwanamke kama kwenye afya, elimu, mila kandamizi, upatikanaji wa mitaji, teknolojia ya kurahisisha kazi, masoko, huduma na ugani, hifadhi ya jamii na unyanyasaji wa aina mbalimbali.
Rais alisema muda umefika wa kufanyia kazi kikamilifu sera na sheria zinazotungwa na mipango inayowekwa kwa ajili ya kuinua hali za kiuchumi ya kuleta ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.
Tunatarajia kuona mabadiliko makubwa ikiwamo Waziri, Naibu na Katibu Mkuu watakaoteuliwa kuendesha wizara hiyo kushirikiana na kamati kutambua changamoto za muda mrefu, ambazo jamii inaona zinaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Pia, tuone mabadiliko kwenye madawati ya jinsia, idara za maendeleo ya jamii ambazo zipo kwenye halmashauri mbalimbali nchini ambazo zinahusika na jamii ngazi ya chini kabisa ili kuona mabadiliko makubwa katika ukatili wa kijinsia, uchumi, maendeleo ya kijamii na ushiriki wa wanawake kwenye ngazi ya uamuzi.
Ndiyo maana tunasema rais anastahili pongezi nyingi kwa kuona jambo hili muhimu kwa maendeleo ya nchi na kulipa uzito, ikiwamo kuunda kamati maalumu ambayo atakutana nayo hivi karibuni, na sasa picha yetu kimataifa itazidi kuwa nzuri.










