Ingawa bado mzunguko wa kwanza wa ligi hizo haujakamilika, ni dhahiri makocha wameshabaini maeneo yanayohitaji kuboreshwa zaidi, lakini kwa Ligi Kuu ya Wanawake ambayo haijaanza kuna baadhi ya timu ziliendelea kuuza wachezaji wao nje ya nchi baada ya dirisha kubwa kufungwa nchini, hivyo huu ni wakati kwao wa kuziba mapengo hayo.
Tayari baadhi ya klabu tangu wiki iliyopita zilianza kutia saini mikataba na wachezaji wapya ambao ni huru na kuanza kuwatumia kwenye mechi za Ligi Kuu, mmojawapo akiwa ni Ditriam Nchimbi aliyemaliza mkataba wake na Yanga na kujiunga na Geita Gold FC.
Tunatambua katika dirisha hili kama lilivyo lile kubwa, pia wapo wachezaji ambao watatemwa ili kutoa nafasi kwa nyota wapya ambao klabu husika zinaamini wanaweza kuzisaidia kutimiza malengo yao msimu huu.
Kutemwa huko hakuwezi kuwa safari ya mwisho kwao kisoka kwani wapo waliokosa nafasi katika klabu kubwa nchini si kwamba hawana uwezo bali wamezidiwa kidogo na wenzao, hivyo ni wakati kwao kujitadhimini na kuna haja ya kufungua milango ya kwenda kupambana zaidi kabla ya dirisha hilo kufungwa.
Katika hilo, tunaushahidi wa kutosha kwa baadhi ya wachezaji ambao wamewahi kuonekana hawafai na kutemwa lakini baada ya kugeuzia mipango yao kwingineko, wakang'ara na baadaye kusajiliwa tena na klabu zilizowatema awali ama kubwa zaidi.
Kwa mantiki hiyo, wachezaji watakaotemwa hawana budi kutambua hayo ndiyo maisha ya soka na kinachotakiwa ni kupambana zaidi kwa klabu zitakazowasajili ili kurejesha ubora wao na hatimaye kujiongezea soko.
Lakiini, tunafahamu wazi zipo klabu ambazo zimetega mitego yao zikisubiri wachezaji watakaotemwa hususan kutoka kwa klabu kubwa ili ziwasajili kabla ya dirisha kufungwa, kwa kutambua hilo, Nipashe tungependa kuona klabu zikitangulia kwanza kutangaza mapema wachezaji zinaowatema kabla ya kuanza kusajili wapya ili kuwapa fursa ya kujiweka sokoni kabla ya dirisha kufungwa.
Pamoja na hayo, huu ni wakati sahihi kwa wachezaji ambao walikuwa hawapati nafasi katika vikosi vyao vya kwanza kuomba kuondoka ili kuokoa viwango na vipaji vyao kwa ujumla.
Tunatambua wapo wachezaji ambao walishawishika kusajiliwa na baadhi ya klabu kutokana tu na kutanguliza maslahi mbele badala ya kumulika pia nafasi zao za kucheza, hivyo kujikuta wakisugua benchi katika kila mechi ama kuishia kupata nafasi chache dimbani.
Wachezaji kama hawa hawana budi kuomba wenyewe kuondoka ama kutolewa kwa mkopo badala ya kuendelea kusugua benchi ama kusubiri kucheza wakitokea benchini kila wakati.
Hatutarajii kuona kunakuwa na klabu zitakazowabania wachezaji ambao hawapati nafasi ya kucheza, watakaomba kuondoka ama kutolewa kwa mkopo kama wanamalengo nao kwa baadaye. Tunayasema hayo kutokana na kutambua kuwa soka ni ajira na biashara kubwa, hivyo, matarajio yetu ni kuona usajili wa dirisha hili kanuni na sheria zikifuatwa, lakini klabu zikitanguliza mbele maslahi ya wachezaji kwanza.










