Rais alitumia mifano yake halisi kuonyesha Jeshi la Polisi lenye wajibu wa kulinda raia na mali zao, limegeuka kuwa maumivu kwa wananchi wengi kwa kutumia nguvu kuumiza wasio na hatia.
Hii ni mara ya pili ndani ya mwaka huu kwa Rais kufikisha ujumbe wenye kuwasilisha maumivu ya wengi dhidi ya matendo yanayofanywa na baadhi ya polisi ambao sio waadilifu.
Rais bila kumung’unya maneno alisema rushwa, matumizi ya nguvu kuliko akili, kuonea watu, kubambikia kesi, kuwapiga, kuwatesa ni miongoni mwa mambo yanayolichafua jeshi hilo na kutaka kufanyike maboresho makubwa ili kurudisha hadhi.
Mifano aliyoitoa Rais Samia ni halisi ya maisha ya watu ya kila siku, na hapo angalau baadhi ya sehemu walimgundua kuwa ni kiongozi wa serikali makali yakapungua, na kama angekuwa raia wa kawaida hali ingekuwa tofauti kabisa.
Mfano aliotumia Rais wa taa ya gari kutowaka hutokea bila dereva au mmiliki kujua, lakini kutokufanyakazi kwa kifaa cha kurusha maji ya kusafishia kioo, lakini unapokamatwa na polisi huwa ni kutozwa faini au umpe rushwa na wakati mwingine hataki kukusikiliza.
Tunatambua kuwa wapo polisi waadilifu wanaofanya kazi nzuri na wengine wamejitoa kusaidia na kuokoa maisha ya wengi bila kujali hali yao na mazingira yoyote na tunaamini wanaochafua jeshi hilo ni wachache ambao wametanguliza tamaa mbele.
Tunathamini na kutambua kazi wanayoifanya ya kupambana na uhalifu wa aina mbalimbali na wapo waliopoteza maisha wakati wakipambana na uhalifu, yote hiyo ni katika kulinda raia na mali zao.
Imekuwa kawaida watu kubambikiwa kesi kubwa kubwa kama za jinai huku wengine wakisota rumande za vituo vya polisi bila kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24 kwa mujibu wa sheria wala dhamana ambayo ni haki ya mtuhumiwa.
Wachache hawa wamegeuka kuwa maumivu kwa wengi hasa kutumia nguvu bila akili, kutesa watuhumiwa ambao wengine hufariki na kupata ulemavu wa kudumu, pia kupokea rushwa na baadhi kudaiwa kujihusisha na uhalifu wa aina mbalimbali kama wizi wa mali za raia na mwingine.
Barabarani nako ni kilio kwa kuwa wananchi hubambikiwa makosa kwa kuonyeshwa kamera za uongo kuwa wametembea kwa mwendokasi na wakati mwingine kutakiwa kutoa rushwa kwa lazima au aandikiwe faini au wengine kuandikiwa faini kwa adhabu ambazo hawajatenda.
Mathalani, kwa sasa kuna mchezo wa kuonea madereva kwenye mistari ya pundamilia, yaani askari wanajificha au kusimama mbele ya mistari kuangalia gari ambalo halijasisimama hata kama hakuna mtembea kwa miguu, gari linatakiwa kusimama.
Wakati mwingine dereva amesimama kwa muda kupisha watembea kwa miguu, lakini anapoondoa gari anasimamishwa kwa kuwa mtembea kwa miguu kajitokeza anataka kupita.
Eneo jingine ni kwenye taa ambazo wakati mwingine hazifanyi kazi hutumika kama kichaka kwamba dereva anaambiwa amevuka kwenye taa nyekundu wakati kiuhalisia sio kweli, na ndiyo maana tunasema ifike mahali kuwe na kamera kwenye taa ambazo zitapiga picha kuonyesha uhalisia.
Ni muhimu sana Jeshi la Polisi likajinasua kwenye hali hii na kujisafisha dhidi ya taswira ya kuwa ni wenye kupenda rushwa, wanaoonea, kumbambikizia watu kesi na kuumiza watu kwa lengo la kuwakomoa kwa kuwa hawajatoa rushwa wanayotakiwa kutoa.
Alichokisema Rais Samia ni uhalisia wa mambo kwenye vituo vya polisi, barabarani na kwingine ambako polisi wanahusika na sasa tunataka kuona mabadiliko makubwa sasa.