Shughuli hizo ni sikukuu ya Krismasi, kufunga mwaka na kuanza mwaka mpya pamoja na wazazi kuwajibika kupeleka watoto wao kuanza shule na wengine kuendelea na masomo.
Kwa maana hiyo Desemba I mwezi ambao watu kadhaa husafiri kutoka eneo moja kwenda lingine kwa ajili ya kuungana na jamaa, ndugu na marafiki kwa ajili ya kusherehekea Krismasi na shughuli za kuufunga mwaka na kufungua mwaka mwingine, hivyo fedha huhitajika kwa ajili ya usafiri na matumizi mengine.
Kwa upande mwingine, hata wasiosafiri huingia katika gharama za kununua mahitaji kama vyakula, mavazi na gharama nyingine. Uzoefu unatuonyesha kuwa kipindi hiki watu huhitaji fedha na hata wengine kukopa.
Mbali na fedha kwa ajili ya sikukuu, pia Desemba ni kipindi ambacho wazazi na walezi hukabiliwa na jukumu la kulipa ada za Januari kwa watoto wanaoanza chekechea, darasa la kwanza na kidato cha kwanza pamoja na wanafunzi wengine wanaorejea shule baada ya likizo.
Watoto hawa sio tu wanahitaji kulipiwa karo pekee bali pia sare za shule na mahitaji mengine ya lazima pamoja na fedha binafsi kwa ajili ya matumizi kwa wanaoishi bweni.
Kwa watu ambao wana utaratibu wa kujiwekea akiba kwa ajili ya shughuli za Desemba na mwisho wa mwaka hawana tatizo, ila wasiokuwa na utaratibu wa kujiwekea akiba kidogokidogo hawa wana shida na kwa vyovyote wanakumbana na shida.
Kuanzia mapema wiki ijayo zitakuwa zimebakia wiki mbili kabla ya Krismasi, hivyo pilikapilika kuanza ikiwamo baadhi ya watu kusafiri kutoka eneo moja kwenda lingine kusherehekea.
Pamoja na umuhimu wa sherehe hizo, ni wajibu wa wazazi na walezi kukumbuka kwamba suala la shule ni muhimu, kwa maana ya gharama zinazohitajika kuwa zimekamilishwa kabla ya mambo mengine.
Elimu ndio uwekezaji na urithi kwa mtoto wake au mtoto anayemlea, hivyo maandalizi ya shule kwa mwakani yanapaswa kukamilishwa mapema ili kujiepusha na usumbufu wa mtoto kukataliwa kupokelewa shuleni kwa sababu za kutokukamilisha mahitaji muhimu.
Gharama za shule haziwezi kuepukwa kwa sababu hakuna mmiliki wa shule ambaye atakubali kumpokea mtoto ambaye hajalipa karo na mahitaji mengine muhimu kwa kuwa shule zinaendeshwa kwa gharama kubwa.
Kutokana na hali hiyo, tunawashauri wazazi na walezi waanze sasa kufanya mandalizi ya kujiwekea akiba kidogo ili Januari ikifika wawe wamekamilisha mahitaji hayo na watoto wao wapokelewe na kuanza masomo bila mkwamo wowote.
Hatusemi kwamba watu wasisherehekee, bali tunashauri wafanye hivyo, lakini kipaumbele kiwe elimu kwa watoto wao, tukiamini kuwa sherehe ni mambo ya kupita tu ila elimu ni suala muhimu na endelevu.
Baadhi ya mataifa jirani zetu yanalitambua hilo, hivyo kuamua kulipa suala la elimu kipaumbele, ikiwamo kuwekeza na kupeana sapoti kupitia michango ya harambee ili kusomesha watoto ikiwamo kuwapeleka ng’ambo.
Ni wakati mwafaka sasa na sisi kama taifa kuona umuhimu wa elimu kabla ya mambo mengine, kwa kutambua kuwa ndio ufunguo wa maisha kupitia kuwekeza katika sekta hiyo kwa urithi wa watoto wetu.










