Mawaziri wazibane bodi za mashirika ya umma

08Dec 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mawaziri wazibane bodi za mashirika ya umma

KUFANIKIWA au kufeli kwa mashirika au taasisi za umma katika utendaji wa majukumu yake kwa kiwango kikubwa ni matokeo ya namna gani bodi za wakurugenzi zinavyosimamia.

Mchango wa bodi hata kwa uendeshaji wa kampuni au shirika binafsi ni mkubwa, kwa kuwa bodi ndizo zinazopanga/kuweka malengo ya kutekelezwa na menejimenti (uongozi), kufuatilia utekelezaji wake na mwishowe kupima matokeo kama malengo yaliyowekwa yametekelezwa.

Kwa majukumu zilizonayo bodi tunaweza kuona kwamba ndizo zenye wajibu katika kuhakikisha kwamba mashirika na taasisi yanafikia malengo kwa tija na ufanisi, kinyume chake bodi zinapaswa kuwajibika.

Ndiyo maana pale shirika au kampuni inapofanya vibaya katika utendaji, bodi inakuwa ya kwanza kuwajibika au kuwajibishwa, ikiwamo kuvunjwa.

Tumeshuhudia mashirika na taasisi nyingi za umma zikifeli katika utekelezaji wa majukumu yake na matokeo yake ni kuisababishia hasara serikali. Matukio haya mara nyingi yamekuwa yakihusishwa na bodi kushindwa kuwajibika katika usimamizi.

Kwa bahati mbaya sana pamoja na mashirika yetu kadhaa ya umma kutofanya vizuri na mengine kufa na kuiachia serikali madeni ya mabilioni pamoja na hasara, chanzo chake hakielezwi wala wajumbe wa bodi hawachukuliwi hatua za kisheria zaidi ya bodi kuvunjwa.

Tunampongeza sana Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, kwa ujasiri wake wa kuliweka sawa jambo hili. Juzi Prof. Mbarawa alifichua jinsi gani wajumbe wa bodi wanavyochangia utendaji mbovu wa mashirika ya umma kutokana na kutowajibika katika kutanguliza maslahi ya umma.

Akizindua Bodi mpya ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), juzi jijini Dar es Salaam, Prof. Mbarawa alisema bodi za mashirika hayo yanapaswa kutanguliza maslahi binafsi na kwamba ndio maana nyingi zinavunjwa kutokana na kushindwa kusimamia ununuzi, maslahi binafsi pamoja na kuendekeza urafiki.

Kwamba nyingi zinashindwa kutimiza majukumu ziliyopewa kutokana na baadhi ya maofisa watendaji wakuu wa mashirika ‘kuwashika’ wajumbe wa bodi, hali inayosababisha kila jambo wanalopelekewa kulipitisha pasipo kuhoji.

Alisema wajumbe wa bodi wengi wanakuwa na maslahi binafsi, hali inayowasababishia kujisahau kutimiza majukumu waliyopewa.

Kwa mujibu wa utaratibu, mwenye mamlaka ya kuteua wenyeviti wa bodi za taasisi na mashirika ya umma ni Rais, huku waziri husika akiwa na mamlaka ya kuteua wajumbe. Kwa misingi hiyo, tunaona kwamba mawaziri wana wajibu wa kusimamia na kuzifuatilia kwa bodi kama zinatimiza wajibu wake sawasawa na inavyotakiwa.

Alichokisema Waziri Mbarawa ndicho kinachoendelea katika mashirika mengi, kutokana na watendaji wakuu ‘kuwashika’ wajumbe kwa maana ya kuwapa ‘bahasha’ na takrima nyingine nyingi ambazo ni kinyume cha utaratibu ili wasifurukute.

Alichokisema Prof. Mbarawa kinaakisi uhalisia wa hali ilivyo kwenye mashirika hayo. Itakumbukwa jinsi baadhi ya mashirika katika miaka ya nyuma yalivyokuwa yakipeleka mikutano ya bodi kufanyikia Afrika Kusini, Dubai na nchi zingine, hivyo kuigharimu nchi mabilioni ya shilingi!

Pamoja na Rais kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kuzivunja bodi, tunaona kwamba njia pekee ya kuyanusuru mashirika yetu na taasisi ni mawaziri husika kuwa wakali na kumshauri Rais kuzivunja bodi inapobainika utendaji unayumba.

Pia tunaona kuwapo haja ya kubadili mitazamo katika uteuzi wa wajumbe wa bodi zetu kwa kuangalia uwezo wa wajumbe ukiwamo ubunifu badala ya kuteua watu kwa ajili ya kuwapa zawadi hata kama umri umewatupa mkono au kuwapa shukrani, vinginevyo hakutakuwapo na tija wala ufanisi katika utendaji.

Ili wajumbe kuwafanya wajumbe wa bodi wawajibike kulinda na kutanguliza mbele maslahi ya umma, serikali ifikirie pia kuweka taratibu za kuwawajibisha kisheria pale wanapobainika kuzembea au kuhusika katika kuisababishia nchi hasara.