Taabu usafiri mabasi idhibitiwe mwezi huu

07Dec 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Taabu usafiri mabasi idhibitiwe mwezi huu

KILA Desemba tumekuwa tukishuhudia kero na taabu ya usafiri wa mabasi katika maeneo mengi hususan kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya kaskazini.

Hali hii hutokana na watu wengi kwenda kusherehekea siku za mwisho wa mwaka za Krismasi na Mwaka Mpya kwenye maeneo wanayotoka, hivyo kuwapo mahitaji makubwa ya vyombo vya usafirishaji hususan mabasi.

Kutokana na hali hiyo, wenye mabasi hukiona kipindi hicho kama fursa kwao ya kutengeneza fedha nyingi na kuamua kupandisha nauli mara dufu, waliamini kuwa lazima abiria watalipa.

Kutokana na mazoea hayo, tunaona kuwa hali hiyo itajirudia kuanzia siku chache zijazo kwa kuwa zimebakia takribani wiki mbili watu wengi kuanza safari kwenda kusherehekea sikukuu hizo.

Wamiliki na wafanyakazi wa mabasi ya abiria yanayosafiri kati ya mikoa na mikoa wameshaanza kujiandaa kunufaika kwa fedha nyingi kupitia kupandisha nauli mara dufu.

Serikali katika miaka ya karibuni imekuwa ikijitahidi kuingilia kati kuhakikisha kuwa wananchi hawaumizwi na vitendo hivyo. Mojawapo ya hatua hizo ni kuruhusu magari madogo kusafirisha abiria kwa kipindi hicho.

Hata hivyo, wakati mwingine magari hayo hayatoshelezi mahitaji, hivyo wasafiri kuendelea kuteseka kwa kukwama kusafiri au kutozwa nauli ya ulanguzi.

Pamoja na kuipongeza serikali kwa kuliona tatizo hilo na kuamua kuingilia kati, lakini tunaona kwamba ipo haja ya kuchukuliwa hatua zaidi kwa lengo la kulitafutia tatizo hilo ufumbuzi wa kudumu.

Miongoni mwa hatua za kuchukua ni mamlaka husika kuhakikisha hakuna basi la abiria linalopandisha nauli kipindi chote cha sikukuu hadi Januari hivyo kuendelea kusisitiza kutumika nauli elekezi.

Pili kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria kwa basi lolote la abiria litakalobainika kupandisha nauli kipindi hicho au kukataa kusafirisha abiria kwenda katika maeneo ambayo limesajiliwa kufanya shughuli za usafirishaji.

Pia kutoa vibali vya muda kwa wasafirishaji zaidi wenye mabasi na magari mengine yanayoweza kusafirisha abiria kwa lengo la kutosheleza mahitaji.

Tunashauri kwamba serikali iangalie uwezekano wa kuongeza safari za treni kwenye mikoa yenye mahitaji makubwa ya usafiri katika kipindi hicho hususan mikoa ya kaskazini.

Ni matarajio yetu kwamba kwa kufanya hivyo usumbufu, taabu na mateso kwa wasafiri katika kipindi hicho itabaki kuwa historia.

Tunaelewa kwamba jukumu la serikali si kuingilia soko katika mfumo wa soko huru, lakini inawajibika kufanya hivyo kwa kuingilia kwa muda mfupi pale inapoona kuna athari kwa ajili ya kuweka mambo sawa.

Kwa hiyo serikali itaonekana kwa wananchi haiwajibiki ikiwa itakaa kimya huku baadhi ya watu wakikiuka sheria kwa makusudi na kuwaimiza wananchi.