Hongera Tembo Warriors, Mungu ibariki Tanzanite

04Dec 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hongera Tembo Warriors, Mungu ibariki Tanzanite

WAKATI Timu ya Soka ya Taifa ya Watu Wenye Ulemavu (Tembo Warriors), ikiandika historia ya kufuzu tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia za mashindano hayo kwa mara ya kwanza, mabinti wa Kitanzania wenye umri chini ya miaka 20 (Tanzanite Queens), nao watashuka dimbani kuvaana na wenzao..

kutoka Burundi.

Tembo Warriors ilipata tiketi hiyo baada ya kuichapa Cameroon mabao 5-0 kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali ya michuano ya Afrika (CANAF), iliyofanyika hapa nchini, ingawa imeshindwa kutinga fainali kufuatia kupoteza mechi iliyofuata.

Tunapenda kuchukua nafasi ya kipekee kuipongeza Tembo Warriors kwa mafanikio ambayo wamefikia kwenye michuano hiyo, na kwa kufanya hivyo watambue wamelipa heshima jina la Tanzania.

Kama ilivyo kwa timu nyingine, Tembo Warriors walikuwa na changamoto mbalimbali, lakini wachezaji wake waliamua kujituma na kuweka mbele maslahi ya taifa.

Kwa kuamini wameingia katika michuano hiyo wanapeperusha bendera ya Tanzania, wanastahili kupewa pongezi na ikiwezekana hata kutunukiwa zawadi mbalimbali kama 'maaskari' wengine walivyopewa ili kuendelea kuwajenga na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kujiandaa na mashindano ya dunia.

Pongezi za Tembo Warriors, haziwezi kukamilika bila kumtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ambaye aliikabidhi timu hiyo kiasi cha Sh. milioni 150 ili ziwasaidie kwenye maandalizi na gharama za kila siku wakati wote wa mashindano.

Motisha hiyo ya Rais Samia ilikuwa na maana kubwa kwa timu hiyo, na kwa kufahamu umuhimu wake, Tembo Warriors walienda kutekeleza kile kilichotarajiwa na Watanzania hasa ukizingatia fainali hizo za CANAF zimefanyika kwenye ardhi ya Tanzania.

Katika hali halisi, sasa Tembo Warriors inahitaji zaidi misaada ya fedha za vifaa kwa ajili ya kufanya maandalizi ambayo yataendana na ukubwa wa mashindano yaliyoko mbele yao.

Rais Samia alifungua njia, huu ni wakati mwingine kwa makampuni, taasisi na wadau wa michezo kuidhamini timu hiyo ili iweze kwenda Uturuki kushindana na si kushiriki.

Ni imani yetu kuwa timu hiyo ikiwa imara, basi itakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kupata matokeo chanya, na hayo yote hayawezi kufanyika bila ya misaada kutoka kwa wadhamini mbalimbali.

Kwa upande wa Tanzanite, leo mchana inashuka dimbani kuwakaribisha wapinzani wao kutoka Burundi katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili kwenye michuano ya kusaka tiketi ya kwenda Costa Rica katika fainali za Dunia zitakazochezwa mwakani.

Huu ni wakati mwingine wa Watanzania kuiombea dua Tanzanite Queens ifanye vyema katika mechi hiyo na baadaye ya marudiano itakayochezwa ugenini Bujumbura ili itimize ndoto za kushiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza.

Tanzanite Queens ambayo ilianza kampeni hiyo kwa kuwaondoa Eritrea, inahitaji kupata ushindi mnono ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele itakaposafiri kwenda Bujumbura kumalizia dakika 90 zilizobakia.

Tukumbuke kuitakia mema Tanzanite, sio tu kutawapa sifa wachezaji, lakini nchi itaendelea kupata heshima katika ngazi ya kimataifa.

Tunawakumbusha wachezaji kuendelea kujituma kwa sababu michuano hiyo ni nafasi nyingine ya kutangaza vipaji vyenu na kwa wale watakaong'ara watakuwa wamejitengenezea 'daraja' la kwenda kucheza soka la kulipwa huko ughaibuni.