Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Ajira, Uratibu wa Bunge, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema tafiti hizo zinaonyesha kuwa maambukizi mapya ya VVU yanawakabili zaidi vijana wenye umri huo ambayo yamefikia asilimia 40.
Aidha, asilimia 80 kati ya hao ni vijana wa kike ambao ni nguvu kazi ya taifa na kwamba katika kukabiliana na hali hiyo serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ukiwamo wa kudhibiti Ukimwi wa mwaka 2018/19 na 2022/23.
Lengo la mpango huo ni kupunguza maambukizi mapya ya VVU, kupunguza vifo vitokanavyo na VVU na kuhakikisha watu wanaoishi na maambukizi ya VVU wanaendelea kutumia dawa.
Pia, alitaka mikoa inayoongoza kwa maambukizi ni Njombe, Iringa, Mbeya, Kagera na Geita huku baadhi ikiwa na kasi kubwa ya maambukizi zaidi ambayo ni Geita, Simiyu, Manyara na Dodoma.
Miongoni mwa jitihada zinazofanywa ni kusambaza kondomu kwenye maeneo ya migodi na uvuvi ikiwamo kutoa elimu ya kujikinga.
Ongezeko hilo la maambukizi kwa vijana siyo habari njema kabisa, bali ni jambo la kushtua linalopaswa kuangaliwa kwa jicho la ziada ili kuhakikisha maambukizi yanashuka au yanakwisha kabisa na kufikia lengo la 2030.
Unapotembelea maeneo mengi ya starehe kama ni bar au disco likiwa ni jipya kidogo kidogo litaanza kupata wadada wanaojiuza ambao ukiwaangalia kwa haraka wako kwenye umri mdogo sana, kiasi cha kujiuliza wazazi au walezi wanajua kinachoendelea dhidi ya watoto wao?
Wasichana hao huwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume tofauti tofauti wengine ni wenye umri sawa na wazazi wao, na wanapotoka hapo huwa na uhusiano na vijana wa umri wao au waliwapita kidogo.
Mathalani, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, ameeleza kukerwa na kuongezeka kwa dada poa, huku akiagiza Wakuu wa Wilaya kuchukua hatua kukomesha hali hiyo.
Uwepo wa dada poa hawa kumefanya ionekane ni jambo la kawaida sana kufanya ngono holela na hadharani, kiasi kwamba unapotembelea mji au jiji lolote unaelekezwa wanapopatikana kiurahisi.
Mbaya zaidi panapofanyika uchafu huo ni mahali ambako kuna uongozi kuanzia ngazi ya mtaa hadi wilaya, ambao wangesimama imara ingesaidi kuwaondoa, lakini wamiliki wa sehemu za starehe wanaona hao wanawasaidia kuvuta wateja ambao ni wanaume.
Ni muhimu takwimu hizi zikatumiwa na wadau mbalimbali kutoa elimu sahihi kwa vijana kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu, lakini kila halmashauri kutoa mtaji na elimu ya ujasiriamali kwa vijana ili wanapomaliza masomo wasikae mtaani bali wajishughulishe na kazi za uzalishaji.
Tunaamini kwa sasa watu wanauchukulia poa Ukimwi tofauti na miaka ya nyuma, sasa ni wakati wa kuongeza kasi ya kutoa elimu sahihi kwa vijana waepuke kuingia kwenye ngono zembe kabla ya umri na wakati sahihi kwenye maisha yao.
Pia ni muhimu elimu ya msingi hadi Chuo Kikuu ikamwandaa kijana kujitegemea kwa kuwa wengi wanaojiuza hutafuta kipato cha kujikimu, na tunaamini kama watajikomboa dhidi ya umaskini na fikra watajitegemea kimaisha.
Bila kuwekeza nguvu kukomboa kundi la vijana kuna hatari kubwa ya maambukizi kuzidi zaidi hasa kwa wanandoa kwa kuwa baadhi huwa na mahusiano na waume au wake za watu ambao huenda kukutana na wenzao wao na kusambaza maambukizi.










