Kutokana na hali hiyo, wanawake walikosa fursa ya elimu, kumiliki mali, kuwa na maamuzi au kushika nafasi za maamuzi, kisiasa hadi kuwa wakuu wa nchi na nafasi nyingine muhimu kwenye jamii.
Siku hii hutumika kutambua, kuthamini na kuenzi mchango wa mwanamke kwa maendeleo ya jamii yake, nchi na dunia kwa ujumla, pia kupaza sauti juu ya changamoto za maeneo yenye kuhitaji marekebisho ili kufikia usawa usio na kikwazo kwa sababu ya jinsia.
Baadhi ya mila na tamaduni zimetumika vibaya kumkandamiza mwanamke kwamba anastahili kuolewa, kumburudisha mume, haruhusiwi kumiliki ardhi au kusema jambo na kusikilizwa. Kutokana na hali hiyo wengi hawakusoma hali iliyosababisha kuwa na wanaume wengi kwenye uongozi kuliko wanawake.
Kauli mbiu ya mwaka huu inalenga kuvunja upendeleo, kwa ajili ya kutoa usawa kwa jinsia zote kushiriki mchakato wa maendeleo na kufurahia maisha kama wengine, pasipo kukandamizwa.
Kwa sasa kuna mabadiliko makubwa kuanzia ngazi ya familia ambazo zimeona umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike na kuondoa dhana kuwa ataolewa hana msaada kwa jamii yake, wapo walioonyesha mfano licha ya kuolewa waliendelea kuzisaidia familia zao na ambao hawakuolewa vile vile wanabeba majukumu ya kutunza wazazi.
Sera na sheria mbalimbali zimetoa haki kwa mwanamke kumiliki ardhi na mali nyingine, lakini bado kuna changamoto kwenye utekelezaji, jamii kutambua na kuchukua hatua.
Kunapokosekana sera ya jinsia eneo la kazi ni rahisi kukuta jinsia moja ndiyo imepewa nafasi za juu, huku wengine wakiachwa katika kuweka usawa ni lazima kuhakikisha wote wanashiriki kwenye ujenzi wa nchi kwa maendeleo endelevu.
Wapo wanaofikiri kuwapa nafasi wanawake ni kuruhusu wanaume wakandamizwe au waonewe, wengine wameenda mbali kuwa wanawake wakishakuwa na nguvu ya kiuchumi wanaacha kuwa watii kwa waume au wakubwa zao, jambo ambalo kimsingi siyo kweli bali hutumika kama mbinu ya kumpunguzia nguvu mwanamke.
Nchi zilizoendelea zimefanikiwa kufikia usawa wa kijinsia kwa kuhakikisha wanawake wanashiriki maendenleo pasipokubaguliwa, wanasoma vizuri, hawalazimishwi kuolewa au kutumika kwa starehe kwa ajili ya mwanaume, lakini wanaongoza kwenye taasisi na mashirika mbalimbali.
Tanzania tumebahatika kuwa na rais wa kwanza mwanamke kutokana na matakwa ya Katiba, tunaamini kwa uongozi wake jamii inakwenda kubadili mtazamo kuwa inawezekana kuwa na rais mwanamke au kiongozi wa nafasi yoyote wa jinsia hiyo.
Haitakuwa ajabu ikiwa mwaka 2025 atagombea nafasi hiyo kwa mujibu wa Katiba, pia wengi watajitokeza kwenye majimbo na kata pasipo kusubiri viti maalum ambavyo mara nyingi vimeonekana ni namna ya kuwapa wanawake upendeleo na siyo kwa sababu wana sifa za kushika nafasi hizo.
Wengi wanatafsiri tofauti ya wabunge wa viti maalum kuwa ni kama mserereko, ingawa kiuhalisia wanapita kwenye chujio mbalimbali kutokana na sifa na vigezo vilivyowekwa na kila chama, lakini kutokana na matazamo wa jamii wanaonekana hawawezi kusimama kwenye majimbo.
Kujiamini hujengwa kuanzia hatua za malezi kwenye familia na jamii inayomzunguka, baadaye shuleni na kazini, tunaamini ni muhimu kuamini ili kufikia agenda ya Umoja wa Mataifa ya 2030 ya kubadili dunia yenye usawa wa kujinsia na ushiriki wa wote kimaendeleo.
Licha ya mafanikio mengi bado kuna kazi kubwa ya kuhakikisha wanawake wanaongoza kwa mujibu wa sifa na vigezo, kuwa na sera na sheria zinazowezesha usawa wa kijinsia.
Pia ni muhimu kufanya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na Sheria ya Mtoto ili zisipingane na Katiba ambayo ndiyo sheria mama kwenye umri wa mtoto, kwa kuwa katika baadhi ya jamii zimetumika kumwozesha mtoto badala ya kupata haki ya kusoma.










