Umuhimu wa kuchukuliwa kwa hatua zaidi za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo unatokana na ukweli kwamba, tishio lake bado lipo nchini hasa kuzingatia takwimu zinazotolewa na serikali juzi.
Tunaamini kwamba Tanzania si kisiwa ambacho hakifikiki, bali ina mwingiliano mkubwa wa watu kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo uwezekano wa usambazaji na maambukizi ya UVIKO-19 yapo.
Kwa kutambua madhara ya ugonjwa huo, serikali ilishatoa waraka wa kuwataka wananchi kuchukua tahadhari zote zikiwamo kunawa mikono kwa maji tiririka, kuvaa barakoa na pia kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
Jambo lingine la msingi linalosisitizwa na serikali, ni wananchi kupata chanjo, lakini bado idadi ya wanaochanja haijaridhisha kutokana na kusuasua, hivyo nasi tunahimiza wananchi kuchukua tahadhari zote ili kuwa salama zaidi.
Juzi Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Aifello Sichalwe, alitoa taarifa kwa umma kuhuusu mwenendo wa ugonjwa wa UVIKO-19 nchini, ikionyesha kuwa watu 33,726 wamethibitika kukumbwa nao, huku 800 wakipoteza maisha kwa kipindi cha Machi, mwaka jana hadi Machi 4, mwaka huu.
Katika taarifa yake ya juzi, Dk. Sichalwe, anasema, idadi hiyo ni kati ya 471,965 sawa na asilimia 7.1 na waliopoteza maisha ni asilimia 2.5 na kwamba kuanzia Februari 5 hadi Machi 4, mwaka huu, kulikuwa na walioripotiwa kupata ugonjwa huo kati ya watu 31,090 waliopimwa na vifo vinane katika mikoa ya Mwanza (5), Dodoma (2) na Kagera (1).
Anasema, katika wagonjwa hao, visa 290 vilivyothibitika, mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na wagonjwa 175 na kufafanua kwamba, kuanzia kipindi hicho cha Februari 5 hadi Machi 4, mwaka huu, wagonjwa wapya 136 walilazwa, kati yao 128 sawa na asilimia 94.1 hawakuchanja na mahututi walikuwa wanne.
Hali hii inadhihirisha kwamba ugonjwa huu bado ni tishio, hivyo sisi kama taifa bado tunalo jukumu kubwa la kuchukua hatua kujilinda na kulindana kama wataalamu wa afya wanavyoelekeza kuhusiana na hatua za kuchukua.
Wakati kukiwa na mwongozo, bado tunashuhudia baadhi ya watu katika maeneo mbalimbali ikiwamo Dar es Salaam, hawauzingatii, badala yake wanakusanyika na kujazana kwenye vyombo vya usafiri wa umma maeneo mengine mengi ya mikusanyiko kama sherehe, masomo, kwenye minada kwa kutaja baadhi. Suala la uvaaji wa barakoa ni kama limeachwa, kwani si jambo la ajabu kukuta ndani ya daladala abiria wamejazana kupita kiasi na hakuna hata mmoja ambaye amevaa barakoa.
Inawezekana kwa mazingira kama hayo, ndiyo maana Dar es Salaam inatajwa tena kwa mara ya pili kuwa kinara wa maambukizi ya ugonjwa huo, ingawa juhudi za kuhamasisha umma kujikinga na ugonjwa huo zimekuwa zikifanyika.
Kimsingi tunashauri, kila mmoja asipuuze maelekezo ya Wizara ya Afya, bali achukue hatua sahihi kuanzia kufuata mwongozo pamoja na kwenda katika vituo kwa ajili ya kupata chanjo, kwani Tanzania si kisiwa kisichofikika.
Tunashauri tahadhari hizo ziende sambamba na uchanjaji, kwani inaelezwa kuwa tangu chanjo ilizinduliwa Julai mwaka jana, hadi kufikia Machi 4, mwaka huu, zaidi ya watu milioni 2.6 tu ndio waliochanjwa. Kwa mujibu wa takwimu hizi, bado tunayo safari ndefu ya kufikia lengo la uchanjaji lililowekwa na nchi yetu la asilimia 60 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu. Ingawa kuchanja ni suala la hiyari, lakini linasababisha watu wanasuasua katika kuchanja.
Hakuna sababu ya kulazimisha watu kuchanja, lakini kwa baadhi ya majirani zetu kama Rwanda ambayo suala hilo ni lazima, wamefanikiwa kuchanja watu asilimia 75, hivyo tunashauri uhamasishaji uendelee kutiliwa mkazo tufikie malengo.










