Juhudi zatakiwa kulibeba soka la wanawake nchini

05Mar 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Juhudi zatakiwa kulibeba soka la wanawake nchini

WAKATI Simba ikiwa ndio klabu pekee hapa nchini imebakia ikipeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, Timu ya Taifa ya Soka ya Wasichana wa umri chini ya miaka 17 kesho inakabiliwa na kibarua dhidi ya wenzao kutoka Botswana.

Wawakilishi hao wa Tanzania watawavaa Botswana kuanzia saa 10:00 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, ni katika mechi ya kwanza ya kuwania tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia za U-17, zitakazochezwa baadaye mwaka huu nchini India.

Timu hizo zitarudiana kati ya Machi 17 na 19, mwaka huu jijini Gaborone na mshindi wa jumla atakutana na kati ya Burundi au Cameroon.

Ni historia isiyofichika kuwa katika kipindi cha miaka 10, timu za taifa za wanawake zimeleta makombe mbalimbali hapa nchini na kuwazidi kaka zao.

Lakini mbali na mafanikio hayo, timu zote za taifa za wanawake ukianza na hii ya U-17, Tanzanite Queens (U-20) na ile ya wakubwa, Twiga Stars, zote zimekosa udhamini.

Mabosi wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), mara kwa mara wamewakaribisha wadhamini kuwekeza katika timu hizo kwa sababu wanaamini endapo nguvu za ziada zitapatikana, basi wanaamini kukosekana udhamini isiwe kikwazo kwa sababu wanaamini ndoto za Tanzania kupeperusha bendera yake fainali za dunia ni rahisi kupitia soka la wanawake.

Umefika wakati makampuni yakaona fahari kudhamini au kuwekeza kupitia mpira wa miguu wa wanawake na hakika kile ambacho watakitoa, kitarejea zaidi lakini wakifurahia mafanikio ambayo yatapatikana kupitia mchango wao wa kusaidia kulipia gharama maandalizi ya timu.

TFF imekuwa ikipambana kuhakikisha timu hizo za wanawake zinakaa kambini kwa wakati, zinapata vifaa lakini ikipambana kuwapa posho wachezaji kwa ajili ya kuwaongezea morali ya kufanya vizuri katika kila mashindano wanayoshiriki.

Tunazikumbusha kampuni na taasisi mbalimbali kuungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan kuwekeza kwenye michezo kuanzia kwenye maandalizi ya timu ili kusubiri matokeo chanya kwa sababu anaamini ili bendera ya nchi ipepee vyema, ni lazima timu au wanamichezo husika wawe walipata maandalizi yanayostahili.

Tunaamini kwa kuwekeza vyema katika kuanzia katika maandalizi ya awali, basi kupata matokeo chanya ndio jambo linalotarajiwa na si kusubiri hadi timu itakapofuzu, ndipo zawadi mbalimbali kuanza kutolewa.

Tuwaamini wasichana au wanawake, kwa sababu njia ya wao kukata tiketi ya kushiriki fainali za dunia ni fupi ukilinganisha na timu za wanaume, lakini ili yote hayo yafanikiwe, fedha na huduma mbalimbali muhimu zinahitajika na hakuna mwingine ambaye anasubiriwa kuwashika mkono U-17 ambao kesho wanakibarua kizito nyumbani na baadaye kurudiana na wapinzani wao huko ugenini Gaborone.

Endapo wadhamini watajitokeza, basi timu hizo zitafanikiwa kupata mechi za kirafiki za kimataifa na michezo hiyo husaidia kuwajenga wachezaji badala ya sasa ambapo wanajipima na timu za wanaume kabla ya kucheza mechi zao za mashindano.

TFF imefungua milango kwa kampuni na taasisi kujitokeza kusaidia timu hizo kwa sababu inaamini nguvu za pamoja zitasaidia kuifanya ndoto ya kucheza Kombe la Dunia inatimia na kila aliyestahili kupongezwa atapata heshima yake.

Tukumbuke mafanikio katika mpira wa miguu yanatokana na uwekezaji unaostahili na kamwe hakuna miujiza au fita za nje ya uwanja. Timu inayopata maandalizi mazuri ndiyo yenye nafasi ya kufanya vyema na si vinginevyo.
Mungu ibariki Timu ya Soka ya Taifa ya Wasichana wa umri chini ya miaka 17. Mungu ibariki Tanzania.