Ndiyo wanaolima takribani asilimia 80 ya vyakula mbalimbali vinavyoliwa katika eneo hilo na hata kuuzwa nje.
Licha ya kinamama kuwa wazalishaji wakubwa wa chakula hapa Tanzania na kwingineko Afrika, suala la kuwa na ardhi wanayoimiliki kwa majina yao bado ni changamoto.
Ndiyo maana tunaamini kuwa kuwapo kwa asilimia 10 ya fedha za halmashauri zinazotolewa kwa wanawake, vijana na wanaoishi na ulemavu kutakuwa na tija zaidi kama tutahakikisha kuwa kinamama wanamiliki ardhi kwa majina yao.
Kwa kuangalia eneo hilo, tunaamini ni wakati wa kuwezesha asilimia 10 ya fedha za halmashauri inayotolewa kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu inavyoweza kutumika kikamilifu kuwekeza kwenye kilimo.
Mahitaji ya mboga, matunda na chakula ni makubwa mno ndani ya nchi iwe mijini na vijijini, lakini hata nje ya mipaka hivyo, kinamama wana fursa kubwa
Tukumbuke kuwa kumiliki ardhi kutawawezesha kupanga na kufanya uzalishaji kwa uhakika zaidi badala ya kutegemea kukodisha . Wanawake wengi mfano mkoa wa Mbeya, Songwe, Morogoro na Pwani wanakodisha ardhi kwa kilimo.
Inamaanisha kuwa kama wangekuwa na mashamba yao pekee huenda wangekuwa mbali zaidi kwenye uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara, ufugaji pamoja na uvuvi.
Tukiwaweka pamoja wanawake na vijana, tunaona kuwa wengi wanashindwa kujikita moja kwa moja kwenye kilimo kwa kutumia fedha za halmshauri za asilimia 10.
Ukweli ni kwamba mikopo hiyo imetumiwa zaidi kwenye biashara kama ya kuuza vyakula (mama lishe), nafaka, matunda na mboga na wengine kufuga kuku.
Wapo wanaojikita kwenye biashara za urembo kama saluni, mavazi , shuka na wengine wakiwekeza kwenye maduka yakiwamo ya kuuza vyombo vya nyumbani na kilimo japo kwa kiwango kidogo.
Ni wazi kuwa ardhi inayomilikiwa kwa pamoja na familia,wana ndugu au ukoo siyo rahisi kijana au mwanamke akaipata na kuitumia kuzalisha bila kufuata mlolongo mrefu ambao pia unatawaliwa na mfumo dume ndani ya familia, jamii na hata mfumo mzima wa ardhi.
Licha ya kwamba hatuna takwimu sahihi , ukweli unabakia kuwa asilimia kubwa ya ardhi ya Tanzania inamilikiwa na wanaume na huenda wanawake wana asilimia mbili pekee na iliyobakia 98 inamilikiwa na wasio wanawake.
Hata hivyo, huu siyo wakati wa kugombea umiliki ila tunachoshauri ni halmashauri nchini ziangalie, uwezekano wa kuanzisha kanda za ardhi ya kilimo kwa kutenga maeneo mahsusi na kuyakodisha kwa masharti nafuu ili wanawake wayatumie kwa kilimo cha mboga, matunda na mazao mengine kwenye halmashauri au wilaya mbalimbali.
Kama ambavyo halmashauri zinatenga ardhi kwa ajili ya uwekezaji (special economic zones) ni vyema kutenga ardhi kwa ajili ya uwekezaji kwenye kilimo kwa ajili ya wanawake hasa wanaokopa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ili waitumie kwenye kuzalisha chakula, mboga na matunda na kuwainua au kuwawezesha zaidi kupitia kilimo wakipitia mikopo ya halmashauri.
Wanawake hawawezi kutumia mali za familia kama ardhi na kuwekeza kama wanavyotamani, ikumbukwe kuwa wanawake hawana haki ya kumilika ardhi na kuzitolea maamuzi hata waume zao wakiwapo na iwapo wenzao hao wamefariki wanakuwa na wakati mgumu.
Ni kwa sababu ni mali ya familia nzima hivyo mama mjane, hawezi kufanya maamuzi ya ardhi ya marehemu mumewe kwa kufanya kile anachopenda hasa kuweka vitega uchumi.










