Ujenzi, ukarabati wa barabara sasa upewe kipaumbele endelevu

22Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ujenzi, ukarabati wa barabara sasa upewe kipaumbele endelevu

BARABARA ni miundombinu muhimu sana katika uchumi na maendeleo ya jamii, hivyo kila wakati kuwa kipaumbele kikubwa kwa wananchi.

Umuhimu wa barabara unadhihirishwa na malalamiko yanayotolewa na wananchi katika maeneo takribani yote nchini kwenye mikutano ya hadhara wanapokuwa wakizungumza na viongozi mbalimbali wakiwamo mawaziri na wawakilishi wao (madiwani, wabunge na wawakilishi).

Wamekuwa wakilalamikia kukosa au kupata huduma hizo zikiwamo za elimu na afya kwa taabu kutokana na ubovu wa barabara, hivyo kuiomba serikali kuhakikisha inazijenga au kuzikarabati mara kwa mara. Hakika barabara ni kikwazo kwa wengi, licha ya jitihada za serikali katika kukabiliana nalo.

Kadhalika, kwenye mikutano ya mabaraza ya madiwani, wabunge na baraza la wawakilishi moja ya huduma ambazo zimekuwa zikiibua mijadala mingi ni barabara, huku madiwani, wabunge na wawakilishi wakipaza sauti kuihoji serikali ni kwa nini haijengi barabara katika maeneo yao na ni lini itafanya hivyo?

Ni maswali ambayo yamekuwa yakiwafanya wahusika kama wakurugenzi na mawaziri kutoa majibu ambayo mara nyingi ni ahadi za kutegemea uwezo wa serikali kifedha pamoja na mipango ya muda mrefu.

Kutokana na kujirudiarudia kwa suala la barabara katika Mkutano wa Bunge unaoendelea, Spika Dk. Tulia Ackson mapema wiki hii alitoa ushauri kwa serikali, pengine baada ya kuona ukubwa wa tatizo hilo.

Jumanne, Dk. Tulia aliishauri serikali kuweka utaratibu wa kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo madogo ya barabara kuepuka gharama kubwa za kuzitengeneza upya.

Ushauri wake ulitokana na swali la nyongeza alilouliza mbunge mmoja wa viti maalum, ambaye alisema serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi katika kujenga barabara, lakini baada ya muda mfupi zinaharibika au kuota nyasi.

Mbunge huyo alihoji kwamba serikali ina mpango gani wa kutenga fedha za matengenezo ya barabara hizo ili kuzinusuru.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya, alisema barabara nyingi za changarawe na vumbi hazidumu kwa muda mrefu na hutengewa fedha kwa ajili ya matengenezo kila mwaka, na kwamba azma ya serikali ni kujenga barabara zote kwa kiwango cha lami. Kasekenya pia alisema ujenzi wa barabara hizo ni gharama na zinategemea upatikanaji wa fedha.

Kutokana na majibu hayo, Spika Tulia aliingilia kati na kusema fedha nyingi zimekuwa zikitumika kujenga barabara hizo, lakini matengenezo huwa hayafanyiki, na kusababisha kuharibika kwa kiwango kikubwa, hivyo kulazimisha kuondoa lami na kujengwa upya.

Tunakubaliana na ushauri wa Spika Tulia kwa serikali kuhusu utaratibu wa kutenga fedha za matengenezo madogo ya barabara kuepukana na baadae kutumika fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo, na wakati mwingine kuchelewa kupata fedha hizo kuwa shida.

Tunaishauri serikali kuanzisha utaratibu huo kwa kuhakikisha Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) zinapatiwa fedha kwa wakati kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao.

Suala lingine linalopaswa kupewa kipaumbele ni kuhakikisha kwamba barabara nyingi zilizoko chini ya TARURA zinafanyiwa ukarabati kwa wakati mwafaka hususan baada ya kipindi cha mvua zinapokuwa zimeharibika.

Tunasema hivyo kutokana na utaratibu mbovu wa barabara hizo kufanyiwa ukarabati wakati wa mvua za masika au vuli, hivyo kupoteza maana halisi ya ukarabati.

Kufanya ukarabati kabla kidogo au wakati wa mvua kunatoa tafsiri kuwa wahusika wana maslahi binafsi badala ya maslahi ya wananchi ambao wanahitaji barabara hizo zipitike kwa kipindi kirefu bila shida.