Masikio, macho, akili zote zaitazama Simba

23Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Masikio, macho, akili zote zaitazama Simba

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania na Afrika Mashariki waliobakia katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba kesho watashuka ugenini Afrika Kusini kuwavaa wenyeji, Orlando Pirates.

Ni katika mechi ya mkondo wa pili wa mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), baada ya kupata ushindi wa bao 1-0, katika mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Simba au Wekundu wa Msimbazi kama inavyoitwa na mashabiki wake inahitaji sare au ushindi wa aina yoyote ili kupata tiketi ya kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo inayofanyika kila mwaka hapa barani Afrika.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wanatakiwa kushuka uwanjani katika mchezo huo kwa nidhamu na kuwaheshimu wapinzani wao kutokana na ubora ambao wanao wanapokuwa nyumbani, lakini pia wakiwa na faida ya kucheza mbele ya mashabiki wao.

Simba inatakiwa kuingia uwanjani ikifahamu inapeperusha bendera ya Tanzania na kwa wao kufanya vyema, si tu kutaibeba jina la klabu yao, lakini kutalipa taifa heshima ambayo imeikosa kwa muda mrefu kupitia michuano hiyo, maana ni muda umepita hakuna timu ya hapa nchini iliyofika hatua ya nusu fainali.

Wachezaji wa Simba wanatakiwa kuingia uwanjani wakisahau bao moja ambalo walipata hapa nyumbani ili kujiweka kwenye mazingira ya kuendelea kupambana na kujipanga kusaka ushindi.

Kama wachezaji wa Simba wataendelea kujituma na kucheza katika kiwango bora kama walivyofanya kwenye mechi zilizopita walipocheza nyumbani, hakika watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupata ushindi na hatimaye kutimiza ndoto na malengo waliyojiwekea ya kucheza nusu fainali au fainali ya michuano hiyo.

Nipashe tunawakumbusha Simba hakuna kisichowezekana, kama iliwahi kuwavua ubingwa wa Afrika vigogo wa Misri, Zamalek tena wakiwa nyumbani kwao, kesho pia inawezekana kwa wao kupata matokeo chanya na hatimaye kusonga mbele.

Huu ni wakati wa Watanzania kuweka pembeni tofauti za kishabiki na kilichobakia ni kuiombea Simba dua njema kwa sababu mafanikio yake pia yataibeba Afrika Mashariki, ambayo kwa muda mrefu timu zake zimekuwa zikitolewa mapema kwenye michuano hiyo ya kimataifa.

Mbali na Simba kuvuna kitita kikubwa cha fedha endapo itasonga mbele, lakini itaihakikishia Tanzania Bara kupata wawakilishi wanne katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika katika msimu ujao, lakini pia Zanzibar ikitoa timu nyingine mbili.

Kimsingi ni jambo gumu kwa wapinzani wao hasa Yanga kuwaombea dua njema, lakini moyoni wanafahamu matunda ambayo Tanzania itayapata endapo Simba itasonga mbele katika michuano hiyo, hivyo ni muda sahihi kwao kuunganisha nguvu kuwaombea watani zao mafanikio.

Katika kuhakikisha Simba inafanya vyema, huu ni wakati mwingine kwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kukaa karibu na wawakilishi hao ili kuhakikisha maandalizi yao ya kuwavaa Orlando Pirates yanamalizika bila ya kuwapo kwa vitendo vyovyote vya hujuma na hatimaye kiu ya kutinga hatua ya nusu fainali inatimia.

Tunafahamu katika mchezo wa soka au mingine yoyote, miujiza ni jambo lisilotarajiwa, lakini huu ni wakati wa kuiombea Simba iwe yenye bahati nzuri kwa siku ya kesho.

Kila mwanamichezo, kwa nafasi yake na imani yake, huu ni wakati wa kuwaombea dua njema Wekundu wa Msimbazi na kuweka pembeni utani wa jadi na upinzani wa ligi ya hapa nyumbani.

Kila la kheri Simba SC, kila la kheri Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.