Stars ikijipanga mapema inaweza kufuzu AFCON 2023

25Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Stars ikijipanga mapema inaweza kufuzu AFCON 2023

TAYARI Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limepanga makundi ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, zitakazofanyika nchini Ivory Coast.

Kwa upande wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imepangwa Kundi F na Uganda, Niger pamoja na vigogo vya soka Afrika, Algeria ambao walitwaa ubingwa huo mwaka 2019 nchini Misri baada ya kuifunga Senegal katika mechi ya fainali.

Katika kila kundi kati ya 12, timu mbili zitakazoshika nafasi ya juu zitakata tiketi ya kwenda kushiriki fainali hizo za juu kabisa kwa ngazi za kimataifa barani Afrika ambazo mwakani zitafanyika kwa mara ya pili nchini Ivory Coast tangu kuanzishwa kwake 1957.

Katika Kundi hilo la F, tayari wengi wanaona nafasi iliyobaki kwa Stars ni moja ambayo itaipigania na Uganda pamoja na Niger huku nyingine wakiitoa moja kwa moja Algeria ambayo imetwaa taji hilo mara mbili, mwaka 1990 na 2019.

Hiyo ni kutokana na ukubwa, uzoefu, uwezo na ubora wa kikosi cha Algeria kinachoundwa na wacheji wengi wanaocheza soka la ushindani barani Ulaya, lakini pia na mlolongo wao wa kufanya vizuri katika michuano hiyo ambayo wametwaa ubingwa mara mbili.

Hata hivyo, pamoja na ukweli huo, bado sisi tunaamini katika soka lolote linaweza kutokea ndani ya dakika 90 kama maandalizi mazuri yataanza kufanyika sasa kwa kila mmoja kutimiza majukumu yake ndani na nje ya kikosi cha Stars.

Imani hiyo tunaipata hasa tukivuta kumbukumbu za hivi karibuni kwa Stars kufanya vizuri ugenini kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya DR Congo, ambao ni miongoni mwa timu imara na zinazoundwa na nyota wengi wanaocheza soka la kulipwa Ulaya.

Stars ilimudu kutoka sare hiyo katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia nchini Qatar baadaye mwaka huu, tena ikiwa haina nyota wake tegemeo, Mbwana Samatta, jambo ambalo linatufanya kuamini katika maandalizi ya mapema na wachezaji kutia nia ya kupambana mwanzo mwisho.

Kwa maana hiyo, hata mechi dhidi ya Algeria, kama Stars ikiandaliwa mapema na wachezaji wakijengewa kujiamini, hakuna kitakachoshindikana ndani ya dakika 180 kwenye mechi ya nyumbani na ugenini.

Kinachotakiwa ni Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen, kuanza kupanga mikakati yake na kuiwasilisha mapema kwa waajiri wake Shirikisho la Soka nchini (TFF), ili kufanyiwa kazi, lakini pia mashabiki na Watanzania kwa ujumla kuwa bega kwa bega katika kuziunga mkono juhudi hizo.

Tunaamini Stars ina uwezo mkubwa wa kupata matokeo ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani wa Benjamin Mkapa, kama Watanzania kwa ujumla watakuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha wachezaji kwa kaulimbiu ambayo imekuwa ikiimbwa na mashabiki wa Simba ya 'Kwa Mkapa Hatoki Mtu'.

Ni wazi kama itaweza kukusanya alama tisa na nyumbani na kwenda kutafuta angalau mbili tu ugenini, inaweza kuwa moja kati ya timu mbili zitakazofuzu fainali hizo kutoka Kundi F, hivyo wakati wa maandalizi ni sasa.

Kinachotakiwa kwa sasa pia ni Poulsen kuzidi kumulika wachezaji hususan wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania kwa kuwapa nafasi zaidi kila anapoita kikosi kwa ajili ya mechi za kirafiki kama alivyofanya kwenye Kalenda ya Fifa iliyopita.

Lakini pia TFF haina budi kuhakikisha katika kila Kalenda ya Fifa, Taifa Stars inacheza mechi za kirafiki mbili ama tatu na moja kati ya hizo ikicheza ugenini ili kuwajengea wachezaji kujiamini wanapocheza nje ya uwanja wao wa nyumbani.

Lengo letu ni kuona Tanzania ikifuzu kwa mara ya tatu katika historia yake kushiriki michuano hiyo, lakini pia ikiigeuza kuwa kawaida kwake kushiriki kila msimu kabla ya kuanza kuweka malengo makubwa ya kufika nusu fainali na hatimaye kubeba ubingwa huo.

Hili litawezekana tu kama maandalizi yatakuwa yakifanyika mara tu kila fainali za msimu husika zitakapomalizika kwa kila mmoja kubeba vema majukumu yake kuanzia viongozi, kocha na wachezaji.